Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema kikosi chake kimeendelea kuimarika kutokana na mazoezi wanayofanya jambo linalompa matumaini kuwa watafanya vizuri kwenye mchezo dhidi ya ZESCO United nchini Zambia
Yanga inajifua kwenye uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo huo utakaopigwa Septemba 28
Zahera amesema wanaendelea kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo wa kwanza, huku akibainisha kuwa wachezaji wameiva
"Kuna mambo mbalimbali tunayafanyia kazi, tunajiandaa kuwa na kikosi bora na imara zaidi ya tulivyocheza mechi ya kwanza, tumejua nguvu yao na tumejua tulipokosea, kikubwa kwa upande wetu, tulishajiandaa kwenda kutafuta goli ugenini, hii ilishakaa kwenye mipango yetu, tukifanikisha, tutakuwa tumefanikiwa," amesema.
Aliongeza kuwa anafurahi kuona kila mchezaji ana morali ya hali ya juu kuelekea mchezo huo wa marudiano na maandalizi ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara watakazokuja kucheza mara baada ya kurejea nchini.
"Timu yetu inabadilika, ninamaanisha wachezaji wanaimarika, kuna tofauti kubwa inaonekana kila siku tunapofanya mazoezi, matumaini yetu ni kuwapa furaha mashabiki wa Yanga na Watanzania wapenda mpira"