Winga wa zamani wa Yanga, Said Maulid ‘SGM’, amesema anaamini watalisaidia benchi la ufundi la timu yao,kufanya vizuri katika michuano mbalimbali, ikiwamo Ligi Kuu Tanzania Bara.
Maulid ni mmoja wa wajumbe wa kamati mpya ya ufundi iliyoundwa na kamati ya utendaji ya klabu hiyo, inayoongozwa na Dk. Mshindo Msolla.
Wajumbe wengine katika kamati hiyo ni Salim Rupia ambaye ni mwenyekiti, Dominick Albinus (makamu) na Charles Mkwasa (katibu).
Wengine Kanali Mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Idd Kipingu, Dk. Jonas Toboroha, Maulid,Keny Mwaisabula, Ally Msigwa, Sunday Manara, Ally Mayay, Sekilojo Chambua na Abeid Mziba ambao ni wajumbe.
SMG amesema viongozi wa klabu hiyo wamewaamini na wakiwapa ushirikiano wanaweza kufanya kazi kwa faida ya timu.
"Tutarajie mambo makubwa kutoka katika kamati hii, kutokana na watu waliopo humu ndani,kuna kitu kikubwa kitafanyika jambola msingi ni kupewa ushirikiano kwa sababu uongozi wenyewe umeona tunafaa,"alisema Maulid.
Kwa upande wake, Charles Mkwasa alisema kamati hiyo itakuwa ikitoa ushauri kwa benchi la ufundi.
Mkwasa alisema benchi la litakuwa na uhuru wa kukubali au kukataa ushauri wao endapo hautawafaa, ila lengo ni moja kuijenga Yanga kiushindani.
"Ni kamati muhimu kwa klabu, uongozi umeona tunaweza kuwasaidia katika eneo hilo kutokana na uzoefu wetu, sisi ni watu tuliokulia hapa Yanga, hakuna kitakachoharibika,"alisema Mkwasa.