Mdau mmoja humu ndani kauliza swali ambalo pengine linaweza kuwafikirisha zaidi wale wanaoamini kutolewa kwa Yanga ligi ya mabingwa tatizo ni kocha Mwinyi Zahera
Tanzania kulikuwa na timu nne zinashiriki michuano ya CAF msimu huu, Yanga Simba, KMC na Azam Fc
Lakini mpaka kufikia jana saa 12 jioni ni timu moja tu iliyobaki kwenye michuano hiyo ambayo ni Yanga
Yanga imeondoshwa kwenye michuano ya ligi ya mabingwa lakini bado ipo kwenye michuano ya CAF kwani inaendelea kombe la Shirikisho
Kama timu ikishindwa lazima kutimua kocha nadhani Simba wangekuwa wa kwanza kumfukuza kocha wao Patrick Aussems kwani wao walitumia gharama kubwa kwa ajili ya michuano hiyo ikiwemo kuweka kambi Afrika Kusini lakini wakatolewa hatua ya awali
Azam Fc inanolewa na Etienne Ndayiragije ambaye ameaminiwa na TFF kuwa kocha wa muda wa timu ya Taifa ya Tanzania, lakini amepoteza mechi zote mbili dhidi ya Triangle United
Kiuchumi Simba na Azam Fc ziko imara zaidi kuliko Yanga, lakini leo hii ni Yanga ambayo bado iko kwenye michuano ya CAF. Hapa bado kuna watu watakwambia tatizo ni Zahera!
Tatizo la sisi mashabiki sio wavumilivu, tunataka mafanikio kwa siku moja. Lazima tukubali Yanga hii ni mpya, zaidi ya asilimia 90 ya wachezaji wa kikosi cha kwanza ni wageni
Pia kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya majeruhi katika baadhi ya nafasi
Wengi tulipenda kumuona Juma Abdul akicheza mechi ya jana badala ya Ally Ally lakini tukiulizana ni lini mara ya mwisho tumemuona Abdul uwanjani?
Miezi mingi imepita, tunajua yuko 'fit' kiasi gani?
Kocha na benchi lake la ufundi ndio wenye taarifa za maendeleo ya wachezaji
Wakati mwingine mchezaji anaweza kupewa majukumu kutokana na sababu za kiufundi kulingana na mechi husika
Yanga ilihitaji kuweka mkazo zaidi kwenye safu ya ulinzi jana ili kukabiliana na presha ya Zesco ambao walikuwa nyumbani
Zahera sio aina ya makocha kama yule wa Simba anayeamini falsafa yake ya kushambulia mda wote lakini mwisho wa siku kwenye mechi kubwa anaishia kufungwa bao tano tano ugenini
Moja ya mambo ambayo Zahera amefanikiwa Yanga ni kutengeneza safu imara ya ulinzi, ambayo imempa uwezo wa kuwa na kikosi kinachoweza kutoa upinzani popote kinapoenda kucheza
cutKuna wakati Yanga ilikuwa ikinolewa na Hans van Pluijm, ilicheza mpira mzuri sana na wakuvutia
Lakini ilipokwenda kwenye michuano ya Kimataifa (kombe la Shirikisho) haikufanya vizuri. Kwa sababu Pluijm hakuwa na mbinu za kushindana kwenye mechi kubwa
Na ndio ikawa sababu ya kuletwa George Lwandamina ambaye naye mwanzoni alipotua Yanga alikumbana na upinzani huu anaokumbana nao Zahera
Lwandamina alikuwa ametoka kuifikisha Zesco nusu fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa, lakini wapo waliompinga kuwa hana uwezo!
Kwa mtizamo wangu naamini bado ni mapema sana wanayanga kukata tamaa
Kufungwa na Zesco isiwe sababu ya kuanzisha mgogoro, lazima kuzingatia mazingira ya timu wakati huu
Hivi karibuni Yanga imeunda Kamati maalum ya ufundi ambayo imesheheni makocha na wataalam wa mpira. Hawa kazi yao ni kumshauri kocha Mwinyi Zahera na benchi lake la ufundi
Naamini wakishirikiana vyema wanaweza kumaliza baadhi ya changamoto zilizopo