Kesho Yanga itashuka dimba la Uhuru kuikabili Polisi Tanzania katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Polisi Tanzania inanolewa na Selemani Matola aliyejiunga na timu hiyo akitokea Lipuli Fc
Matola amekuwa na takwimu nzuri kwenye michezo ambayo timu zake zimechuana na Yanga
Wakati akiwa Lipuli Fc msimu uliopita, Matola alishinda michezo miwili na kufungwa mchezo mmoja
Na hata baada ya kujiunga na Polisi Tanzania, Matoka aliiongoza timu hiyo kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa kirafiki uliopigwa mkoani Kilimanjaro
Kocha Mwinyi Zahera anafahamu changamoto iliyoko mbele wakati timu yake ikijiandaa na kuikabili Polisi Tanzania hapo kesho
Matola ametamba kuzibaini mbinu za Zahera hivyo kuahidi kuendeleza wimbi la ushindi dhidi ya Yanga kesho
Lakini ni mchezo ambao Yanga inahitaji kushinda hasa ikizingatiwa ilipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Ruvu Shooting
Kesho Polisi Tanzania watakumbana na Yanga iliyo imara
Yanga ambayo itataka kumaliza machungu baada ya kuondoshwa michuano ya ligi ya mabingwa na kushushwa kombe la Shirikisho
Pia utakuwa mchezo ambao mshambuliaji Mcongomani David Molinga atataka kuendelea kuwanyamazisha wakosoaji wake
Molinga alifunga mabao matatu jijini Mwanza kwenye michezo ya kirafiki dhidi ya Pamba na Toto Africans wakati timu hiyo ikijiandaa na mchezo dhidi ya Zesco
Wakati wenzie wakielekea nchini Zambia, yeye alibaki jijini Dar es salaam akiendelea na mazoezi