Wiki iliyopita kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera aliwahakikishia mashabiki wa timu hiyo kuwa mshambuliaji David Molinga atafunga zaidi ya mabao 15 kwenye ligi msimu huu
Zahera alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na waandishi wa habari waliohoji mwenendo wa Mcongomani huyo aliyesajiliwa na Yanga siku ambayo dirisha la usajili lilifungwa
"Makambo (Heritier) mnaemsifia sana hapa Tanzania, kwenye ligi ya Congo alifunga mabao saba, Molinga alifunga mabao 15 msimu uliopita kwenye mashindano yote"
"Nakuambia Molinga atafunga mabao 15 mpaka 20 msimu huu, asipofanya hivyo nitatoa dola efu moja kukupatia mwandishi.."
Leo Yanga itakuwa uwanja wa Uhuru kumenyana na Polisi Tanzania, macho na masikio ya Wanayanga yakielekezwa kwa Molinga
Katika michezo yake miwili ya mwisho aliyoichezea Yanga, Molinga alifunga mabao matatu hiyo ikiwa ni ishara kuwa mshambuliaji huyo ameanza kuonyesha makali yake
Molinga alipewa program maalum ya kupunguza uzito na Zahera ambapo mshambuliaji huyo alifika nchini akiwa na kila 84 lakini sasa ana kilo 74 akipungua kilo 10!
Ushindi wa Yanga leo utakuwa mikononi mwake hasa ikizingatiwa yeye hakuwa sehemu ya kikosi kilichosafiri Zambia kwa ajili ya mchezo wa ligi ya mabingwa