Oktoba 27 Yanga itakuwa nyumbani dimba la Taifa kuikabili Pyramids Fc kutoka nchini Misri ukiwa mchezo wa kwanza kombe la Shirikisho kusaka nafasi ya kutinga makundi
Kutokana na kufahamu fitna za timu za Misri zinapocheza kwao, Yanga inapaswa kupata ushindi mnono kwenye mchezo huo wa nyumbani
Msemaji wa Yanga Antonio Nugaz amesema wanafahamu nini wanapaswa kufanya kwenye mchezo huo ili kuwa na nafasi ya kutinga hatua ya makundi
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Nugaz amesema pamoja na kuwa Pyramids ni timu ngeni kwenye michuano ya CAF, lakini wanaiheshimu
Amesema Yanga haitishwi na takwimu za uwekezaji wa klabu hiyo pamoja na wachezaji ghali walionunuliwa kwani mpira wa miguu huchezwa uwanjani na matokeo hupatikana baada ya dakika 90
"Katika kuelekea mapokeo ya Pyramids sisi kama Yanga hatudharau, hatuchukulii poa wala hatuoni kwamba ni timu ndogo kwa kuwa ndio kwanza inashiriki," amesema
"Lakini pia hatutishwi na vigezo vya uwekezaji kwani mpira unachezw uwanjani. Sisi tunatakiwa tuwaonyeshe mechi iishie hapahapa"
"Tunawapiga tano hapa halafu kule kwao tunakwenda kukamilisha ratiba tu"
"Wanayanga wana kila sababu ya kujiamini na kutembea kifua mbele kwani Yanga ndio timu pekee iliyobaki kwenye michuano ya Kimataifa kutoka Tanzania, hakuna mwingine"
Katika maandalizi ya mchezo huo, Yanga inatarajiwa kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Friends Rangers na Pan Africans kisha kuelekea mkoani Mwanza kuikabili Mbao Fc ukiwa ni mchezo wa ligi kuu