Baada ya Yanga kupangwa na Pyramids Fc, kumekuwa na msululu wa takwimu zinazotolewa na wachambuzi wa soka nchini kuhusu utajiri wa klabu hiyo pamoja na matokeo yao katika michezo iliyopita
Lakini wengi wanasahau jambo lolote linaweza kutokea kwenye mpira wa miguu muhimu ni kufanya maandalizi ya kutosha
Mwaka juzi Yanga ilitinga makundi ya michuano ya kombe la Shirikisho kwa kuitoa Wolayta Dicha ya Ethiopia
Kwa wanaokumbuka Wolayta Dicha iliiondoa Zamalek na kupata nafasi ya kutinga hatua ya mtoano
Kabla ya mchezo huo takwimu nyingi zilitolewa hasa baada ya Dicha kuichapa Zamalek
Walipokuja uwanja wa Taifa, Waethiopia hao walikubali kipigo cha mabao 2-0, mabao ya Raphael Daudi na Emmanuel Martin
Wakati huo Yanga ilikuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi sana lakini kocha George Lwandamina aliiandaa timu yake vyema na ikafanikiwa kushinda kwa matokeo ya jumla ya 2-1 licha ya kufungwa 1-0 nchini Ethiopia
Hata msimu huu Yanga ilikuwa haipewi nafasi ya kuvuka raundi ya awali ya michuano ya ligi ya mabingwa baada ya kupangwa na Township Rollers ambayo mwaka mmoja nyuma iliiondoa Yanga kwa ushindi waliopata uwanja wa Taifa
Hata matokeo ya sare ya bao 1-1 ya mchezo wa kwanza, yalipelekea wengi kuamini Yanga itafungwa bao nyingi ugenini
Lakini kilichotokea kwa Township Rollers imebaki historia
Aidha baada ya mchezo dhidi ya Zesco, kocha wa timu hiyo George Lwandamina alikiri timu yake ilipata bahati kutinga hatua ya makundi huku akiitabiria Yanga kufanya vizuri kwenye kombe la Shirikisho
Msimu huu pamoja na kutofanya vizuri kwenye michezo ya awali ligi kuu, Yanga ni timu tofauti kabisa kwenye michuano ya CAF
Ilienda kushinda Botswana ikitoka kufungwa na Polisi Tanzania 2-0 kwenye mchezo wa kirafiki
Ikapata sare dhidi ya Zesco United jijini Dar es salaam ikitoka kufungwa na Ruvu Shootinga 1-0 kwenye ligi
Pamoja na kupoteza mchezo Zambia, lakini mchezo mzuri walioonyesha uliwafanya Wazambia hao wakose amani kwa dakika zote 90
Wapo wanaobeza kuwa Yanga haipaswi kucheza mechi za kirafiki na timu za daraja la pili wakati inakabiliwa na mchezo mgumu Oktoba 27
Labda niwakumbushe, Yanga hii hii iliweka kambi mkoani Morogoro ikacheza na timu za mtaani lakini leo ndio timu pekee iliyobaki kwenye michuano ya CAF
Mjiulize wale walioweka kambi nje na kucheza mechi kubwa kubwa ziliwasaidia nini?