Kasi ya upachikaji mabao ya mshambuliaji David Molinga imeongeza matumaini ya Yanga kuelekea mchezo wa play-off kombe la Shirikisho dhidi ya Pyramids Fc ambao utapigwa Oktoba 27 uwanja wa CCM Kirumba
Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) limeihakikishia Yanga kuwa wataruhusiwa kumtumia mshambuliaji huyo pamoja na beki Mustafa Suleyman ambao walikosa mechi za awali za ligi ya mabingwa baada ya usajili wao kuchelewa hivyo kukosa leseni za kushiriki michuano hiyo
Ujio wa Molinga umepunguza changamoto ya mabao ambayo imeitesa Yanga tangu mechi za awali
Mpaka sasa Molinga amefunga mabao saba, mawili akifunga ligi kuu na matano akiyafunga katika michezo ya kirafiki
Alifunga bao moja kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Pamba Fc, mabao mawili dhidi ya Toto Africans na jana akifunga mabao mawili dhidi ya Friends Rangers
Lakini pia alifunga mabao mawili kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Polisi Tanzania
Mshambuliaji huyo ambaye kwao Congo anafahamika zaidi kwa jina la Falcao, ana uzoefu wa michezo ya Kimataifa hivyo uwepo wake ni silaha muhimu ya kuimaliza Pyramids Fc jijini Mwanza
Molinga alianza maisha yake katika klabu ya Yanga kwa kusuasua lakini ni dhahiri kasi yake ya kuzifumania nyavu imekuwa ikiongezeka siku hadi siku