Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla amesema hawatakuwa na tatizo kumrejesha kiungo wao wa zamani Haruna Niyonzima kama kocha Mwinyi Zahera atamuhitaji
Baada ya hivi karibuni Niyonzima kukutana na mmoja wa mabosi wanaohusika na masuala ya usajili Yanga, Abdallah Bin Kleb, kumekuwa na taarifa kuwa Niyonzima anaweza kurejeshwa wakati wa usajili wa dirisha
Mwenyewe Niyonzima ameeleza kuwa tayari kurejea Yanga, akikiri kuwa ni klabu aliyoitumikia kwa mapenzi makubwa
Dk Msolla amesema pamoja na kuvutiwa na kiwango cha nyota huyo, hatma yake iko mikononi mwa Zahera
"Ipo wazi Niyonzima aliitumikia Yanga kwa mapenzi yote na alifurahia uwepo wake katika klabu"
"Suala la kama tutamsajili au la litategemea na maoni ya kocha kwani yeye ndiye anayefahamu mapungufu ya timu yake"
Kwa mara ya kwanza, Niyonzima alitua Yanga mwaka 2012 akitokea APR na kufanikiwa kushinda mataji manne ya ligi kuu
Mwaka 2017 alijiunga na Simba klabu aliyoitumikia kwa misimu miwili na kuongeza mataji mengine mawili ya ligi kuu