Pamoja na misukosuko inayomkabili, Mkufunzi wa Yanga Mwinyi Zahera ana wastani mzuri wa matokeo tangu alipotua Yanga
Zahera aliyeanza rasmi kuitumikia Yanga msimu uliopita, ameiongoza timu hiyo katika jumla ya mechi 51 za kimashindano
Msimu uliopita aliiongoza Yanga kwenye mechi 38 za ligi na mechi nne za kombe la FA
Msimu huu tayari ameiongoza Yanga kwenye mechi nne za ligi, mechi nne za ligi ya mabingwa na mechi moja ya kombe la Shirikisho
Katika mechi hizo 51, Zahera ameshinda mechi 33, ametoka sare mechi nane na amefungwa mechi 10
Ana wastani wa kushinda hadi mechi saba katika kila mechi 10 anazocheza
Huu sio wastani mbaya sana kwa kocha
Pamoja na kutofanya vizuri sana kwenye michuano ya Kimataifa msimu huu (ingawa kwa timu za Tanzania yeye ndiye aliyefanya vizuri zaidi), bado hatuwezi kusema matokeo yake ni mabaya kwenye ligi kwani katika mechi nne, ameshinda mbili, sare moja na kupoteza moja
Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga Charles Mkwasa ambaye ni Katibu wa Kamati ya ufundi ya Yanga, amesema mechi nne hazitoshi kumuhukumu Zahera, pengine tathmini nzuri ifanywe angalau baada ya mechi 10