Yanga wakimalizana na Zahera wajitathmini wao

Shabiki NambaMoja By Shabiki NambaMoja
β€’
1 Nov 2019
Yanga wakimalizana na Zahera wajitathmini wao

Imeandikwa na Khatimu Naheka

Hali haijatulia pale ndani ya klabu ya Yanga. Hakuna mtu anayeishi mapigo yake ya moyo yakienda kwa kasi kama kocha wao Mwinyi Zahera, ghafla amegeuka kuwa adui namba moja kwa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo achilia mbali viongozi wake ambao hawajajua washike wapi mpaka sasa.

Kinachowaumiza mashabiki wa Yanga ni hali ya kikosi chao hawaoni kama ni timu ambayo inaweza kufanya kitu, tofauti na lawama kubwa kama ambavyo nimekuwa nikisema hakuna mwingine zitarudi kwa Zahera ambaye hukumu yake inakuja kupitia kauli zake za msimu uliopita kwamba mambo yatabadilika kama usajili mkubwa utafanyika ndani ya klabu hiyo na wanachama wachange fedha zitakazosaidia usajili huo.

Usajili ulipofanyika tayari kuna kauli nyingine ikaibuka juzi kwamba usajili uliofanyika haukuwa kwa malengo ya mashindano ya Afrika, bali ni wa ligi na kauli hii imezidi kuwachanganya zaidi wanachama na mashabiki wake ambao wakiangalia hata katika ligi nako bado hakuna matokeo mazuri.

Nilimkumbusha Zahera kwamba kupitia ahadi zake zile zingekuwa afya tu endapo angekuwa anawapa raia wenzake wa Ulaya ambao wanajua uvumilivu kama ule anaoendelea kuupata kocha wa Everton, Marco Silva ambaye baada ya kufanya usajili mkubwa mpaka sasa bado hajaweza kuonyesha kiwango chochote akipokea vipigo.

Hapa Tanzania ni tofauti na sioni kama Zahera endapo atapata matokeo mabaya katika mchezo wa Pyramids kule Misri, kisha kupata hata sare hapa nyumbani katika Ligi Kuu Bara kama ataendelea kuwa wa Yanga, kuna hali mbaya inaweza kutokea

Uhai wa ajira ya Zahera ndani ya Yanga ni suala la muda, vinginevyo mambo yabadilike kwa haraka kwa kushinda na hatua mbaya zaidi ni kwamba hata baadhi ya viongozi wake nao wanamezwa na nguvu ya wafuasi wao kwa kuishi ndani ya kivuli cha Zahera.

Hakuna namna suala la Zahera kuondoka limebakiza hitimsho, lakini hiyo inaweza kuwa hatua moja kwa Yanga kuanza kutatua changamoto wanazokutana nazo sasa ndani ya klabu yao.

Lakini swali ambalo wengi wanapaswa kujiuliza, je kuondoka kwa Zahera kisha akaja kocha mpya atakuwa na afya gani ya kurudisha heshima ya klabu hiyo?

Nionavyo mimi safari ya kuirejesha Yanga yenye afya bado ni ndefu na inawezekana kama Yanga wakimalizana na Zahera kabla ya kuanza safari mpya na kocha mwingine wajifanyie tathimini nzito katika uongozi wao.

Inawezekana kabisa mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla akawa hajui lakini ni vyema akasimamisha safari kwanza kisha kuwafanyia tathimini wanajumuiya wenzake katika safari yao kwani kuna uwezekano mwisho wao ukawa si mzuri kama ambavyo mambo yanakwenda sasa.

Changamoto ndani ya uongozi wao zimeanza kuwa nyingi, huku mambo mengi yakibaki kwao wakiona kama ni sifa kutoyaweka bayana badala ya kuwaambia ukweli wanachama ambao waliwapa dhamana ya kuongoza kabla ya mambo hayajabadilika zaidi.

Naona utafika wakati yanaweza kuibuka mambo mazito kuliko haya ya Zahera ambayo yatakuja kuiingiza Yanga katika vurugu zaidi na kupoteza ramani nzima ya safari ya uongozi wao uliobeba matumaini mengi.

Wapo ambao wanajionyesha kama wanamsaidia sana Msolla, lakini hali halisi haipo hivyo, wanaishi ndani ya klabu hiyo kwa kutaka kunufaika na mambo yao wanayoyafanya ambayo wasiwasi wangu ndio hatari zaidi kuliko haya ya Zahera ambayo yanashika hatamu sasa.

Kuna harufu kali ya mambo ndani ya uongozi wa Msolla kuanza kupenya katika pua za wanaoizunguka ambazo ni muhimu zikapewa jicho makini katika kuzifanyia kazi ili kurudisha nidhamu halisi ambayo imekusudiwa.

Hili likiachiwa linaweza kuleta shida zaidi na kuleta picha mbaya na hata kuharibu imani ambayo wanachama ambao waliamini sasa klabu yao imeingia katika safari tulivu ya kufika nchi ya ahadi ambayo wanalenga kufika.

Hili la Zahera sina mashaka nalo kabisa litapita kwa urahisi na sioni kama Mkongomani huyo anaweza kushindana nalo na kushinda, lakini pia inawezekana akaamua kufa na wengi kama akija kuinua mdomo wak.

Lakini ni wakati mzuri sasa kama ataondoka, basi hata uongozi nao ujitathimini katika maisha yao kabla ya kumleta kocha mpya ndani ya klabu hiyo.

Mwanaspoti

ADVERTISE HERE

Yanga SC Stories

Kikosi : Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Kikosi : Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
2h ago
READ MORE β†’
Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
Yao bado kidogo, Diarra tayari kurejea
7h ago
READ MORE β†’
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Matchday; Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
10h ago
READ MORE β†’
Yanga inahitaji utulivu, si vita ya lawama
Yanga inahitaji utulivu, si vita ya lawama
11h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
13h ago
READ MORE β†’
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
22h ago
READ MORE β†’
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
1d ago
READ MORE β†’
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
1d ago
READ MORE β†’
Yanga mpya kuanza na Mashujaa Fc, hivi hapa viingilio
Yanga mpya kuanza na Mashujaa Fc, hivi hapa viingilio
1d ago
READ MORE β†’
Hersi akimpata huyu wamekwisha!
Hersi akimpata huyu wamekwisha!
1d ago
READ MORE β†’