Mabingwa wa kihistoria Tanzania, Yanga wako nchini Misri ambapo usiku wa leo Jumapili Novemba 03 2019, watashuka katika uwanja wa 30th June kuikabili Pyramids Fc ukiwa ni mchezo wa kombe la Shirikisho kusaka nafasi ya kutinga makundi
Mchezo huo ni wa pili baina ya timu hizo baada ya Pyramids Fc kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Mwanza
Hivyo Yanga wanahitaji matokeo ya ushindi wa kuanzia mabao mawili ili kuwa na nafasi ya kutinga makundi
Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema wamejipanga kikamilifu na wana matumaini ya kupata ushindi
Amesema wamezifanyia kazi changamoto zilizowanyima ushindi kwenye mchezo wa kwanza, wana kila sababu ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo
Aidha, ari ya wachezaji nayo iko juu. Nahodha Papy Tshishimbi amesema watapambana kuhakikisha wanapata matokeo ili kuweza kutinga makundi
Amewataka mashabiki wa Yanga kuwapa sapoti na kuwaombea ili waweze kushinda
Jana usiku Yanga ilifanya mazoezi katika uwanja wa 30th June ambao mchezo huo utapigwa

Wachezaji walipata nafasi ya kupata uzoefu wa uwanja huo ambao unachukua mashabiki 30,000
Kila la kheri Yanga, kila la kheri Wawakilishi wa nchi..