Mabingwa wa kihistoria Tanzania Yanga leo wametakata uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara baada ya kuichapa Ndanda Fc bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Wakicheza kwa mara ya kwanza chini ya Charles Mkwasa kocha wa muda, Yanga walifunga bao pekee la ushindi kwenye dakika ya 75 kupitia mpira wa adhabu uliowekwa kimiani na Patrick Sibomana 'PS'
Mwamuzi Hans Mabena alitoa adhabu hiyo baada ya Mrisho Ngasa kumnawisha mpira beki wa Ndanda Fc karibu kabisa na mstari wa 18
Awali adhabu hiyo ilipigwa na Molinga lakini Mabema aliamuru mpira huo upigwe tena baada ya wachezaji wa Ndanda kutoka kwenye ukuta kabla ya mpira
Mkwasa leo alifanya mabadiliko madogo kwenye kikosi chake ambapo aliwapanga wachezaji katika namba zao wanazocheza siku zote
Katika safu ya ulinzi Mkwasa alimrudisha Ally Mtoni kucheza kati sambamba na Kelvin Yondani huku upande wa kushoto akimpanga Jaffar Mohammed ambaye leo alikuwa na mchezo mzuri sana
Aidha nahodha Papy Tshishimbi alimrejesha kucheza namba sita huku Mapinduzi Balama akimchezesha namba nane

Tshishimbi na Balama walitawala vyema safu ya kiungo wakiweza kuchezesha timu vyema licha ya changamoto ya ubora wa uwanja wa Nangwanda
Yanga ingeweza kuondoka na ushindi mnono zaidi kama nafasi walizotengeneza kwenye kipindi cha kwanza kupitia kwa David Molinga na Sibomana wangezitumia
Ushindi huo umewahakikishia Yanga kuondoka na kitita cha Tsh Milioni 10 zilizotolewa na wadhamini, GSM
Aidha ni matokeo mazuri kwa Mkwasa 'Master' ambaye ameanza kwa ushindi
Ushindi huo pia umeacha shangwe kwa mashabiki wa Yanga mkoani Mtwara ambao walijitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu yao
