Baada ya kufanya vizuri kwenye mchezo wake wa kwanza, baadhi ya wadau wametoa maoni kuwa ni vyema akaachiwa majukumu ya kuiongoza Yanga mpaka mwishoni mwa msimu
Hapa tunamzungumzia kocha Charles Boniface Mkwasa 'Master' ambaye aliteuliwa kuwa kocha wa muda wiki iliyopita kuchukua nafasi ya Mwinyi Zahera aliyeonyeshwa mlango wa kutokea na uongozi wa Yanga
Mkwasa aliongoza Yanga kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Ndanda Fc ambao mabingwa hao wa kihistoria waliibuka na ushindi wa bao 1-0
Pamoja na kuwa Yanga ilishinda kwa bao 1-0 mechi zilizopita kwenye ligi wakati ikiwa chini ya Zahera, kinachomfanya Mkwasa apigiwe chapuo ni maboresho aliyoyafanya ndani ya muda mfupi
Katika mchezo dhidi ya Ndanda Yanga ilicheza tofauti kabisa, ilikuwa kama timu mpya
Kasi ya uchezaji ilionekana, wachezaji walionyesha uchu wa kusaka ushindi
Timu haikuzidiwa hata pale ilipofunga bao la kuongoza. Siku za nyuma ilikuwa ngumu sana kuitizama Yanga ikicheza hasa pale inapokuwa inaongoza, muda mwingi wapinzani walikuwa langoni kwa Yanga
Pia katika mchezo huo Yanga iliwakosa baadhi ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza ambao walikuwa majeruhi
Yanga iko kwenye mchakato wa kusaka kocha mkuu ambaye atapewa majukumu ya kudumu
Lakini kwa mwanzo huu wa Mkwasa, ni dhahiri uongozi wa Yanga unaweza ukasubiri kuona nini kitatokea
Kwani kama atafanikiwa kuiweka timu katika mstari halafu akaondolewa, Yanga itakuwa kama inaanza tena upya
Kinachopaswa kufanywa na uongozi wa Yanga ni kumtimizia Mkwasa mahitaji ya kikosi chake hata kama wanaendelea na mchakato wa kusaka kocha wa kudumu
Uamuzi wa kuajiri kocha mpya utegemee na mwenendo wa timu wakati huu ambao iko chini ya Mkwasa
Kama timu itafanya vizuri, haitakuwa vyema kufanya mabadiliko ya benchi la ufundi
Kote duniani, makocha wa muda hupewa majukumu ya moja kwa moja pale timu zinapokuwa zinafanya vizuri