Winga wa Yanga, Mrisho Ngassa, amesema bado ana ndoto ya kujerea Taifa Stars, akiamini ipo siku ataitwa katika kikosi hicho.
Taifa Stars leo inatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Mustapha Ben Jannet, Tunisia kucheza na Libya katika mchezo wa Kundi J wa kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2021), zitakazofanyika Cameroon.
Ngasa, mmoja wa wachezaji wa kutegemewa kwenye kikosi cha Yanga msimu huu,amesema kabla ya kustaafu kucheza soka ya ushindani ipo siku atapata nafasi ya kuitumikia Taifa Stars.
Ngasa amesema atahakikisha anamshawishi kocha wa Stars Etienne Ndayiragije kwa kuonesha kiwango katika klabu yake ili aweze kumwita katika kikosi chake.
Amesema pamoja na kikosi cha sasa cha Stars kinaundwa na wachezaji wengi wenye damu changa, lakini wakongwe na wazoefu wana umuhimu wake kuitwa kulisaidia taifa.
"Muda ukifika nitahitajika tena Taifa Stars na nitaenda," amesema
Ngasa ndiye mfungaji bora wa muda wote wa timu ya Taifa, ambapo rekodi yake ya kupachika mabao 25 bado haijavunjwa
Tangu arejee Yanga msimu uliopita, kiwango chake kimekuwa kikiimarika
Juzi kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Coastal Union, Ngasa alifunga bao la 'kideoni', akiachia kombora kali nje ya 18 ambalo lilitinga kambani na kuisawazishia Yanga ambayo ilishinda mchezo huo kwa mabao 3-1