Kiungo mshambuliaji wa Yanga Deus Kaseke amesema mabadiliko ya kikosi cha Yanga chini ya Charles Mkwasa yanatokana na mabadiliko ya mbinu
Kaseke ambaye jana aliisaidia Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya JKT Tanzania, amesema tofauti kati ya aliyekuwa kocha wao Mwinyi Zahera na Mkwasa ni mbinu wanazotumia
"Wote ni makocha wazuri lakini kila mmoja ana mbinu zake. Wakati wa Zahera tulikuwa tunacheza kufuatana na mpango wake na hata sasa tunacheza kufuatana na mpango wa Mkwasa ndio maana tunaonekana tofauti," alisema Kaseke baada ya mchezo
Aidha akizungumzia changamoto ya washambuliaji kukosa ufanisi wa kutumia nafasi zinazotengenezwa, Kaseke alisema ni jambo amalo linapaswa kufanyiwa kazi lakini mpaka sasa wanajitahidi
"Kwa mshambuliaji inapaswa ukipata nafasi mbili utumie angalau nafasi moja.. pamoja na kukosa baadhi ya nafasi lakini washambuliaji wote leo wamefunga hivyo nadhani wanajitahidi"
Kaseke jana aliibuka nyota wa mchezo akihusika katika mabao yote matatu yaliyofungwa na Yanga
Alitoa pasi za mabao yaliyofungwa na Patrick Sibomana na Juma Balinya na pia akafanyiwa madhambi ambayo yalisababisha mpira wa adhabu uliowekwa kimiani na David Molinga 'Falcao'