Kocha wa zamani wa Yanga Mwinyi Zahera amepeleka malalamiko shirikisho la soka duniani (FIFA) baada ya uongozi wa Yanga kuchelewa kukamilisha malipo yake
Zahera alifutwa kazi na Yanga mwezi uliopita baada ya uongozi wa timu hiyo kutoridhishwa na mwenendo wa timu chini yake
Mcongomani huyo yuko nchini kwa kile alichodai kufuatilia malipo yake ingawa kwa nyakati tofauti alibainisha kuwa ataweka makazi yake nchini ili kufungua Academy ya soka
Uongozi wa Yanga umesema hauna fedha za kumlipa kwa mkupuo Mcongomani huyo
Yanga ina malimbikizo ya madeni ya makocha wa nyuma wakiwemo Hans van Pluijm na George Lwandamina
Hata hivyo Zahera amesema Yanga walipaswa kufahamu ni wapi watapata fedha za kumlipa kabla ya kuvunja mkataba wake
"Nimeshafuata taratibu zote kwani najua walitakiwa wanilipe mapema baada tu ya kusitisha mkataba wangu," amesema
"Wanasema hawana hela sasa tutajua, maana makocha wote waliofukuzwa wakiwemo wale wa Simba na Azam FC walilipwa pesa zao siku hiyo hiyo maana huwezi kufanya maamuzi bila kujua utatoa wapi pesa"
Mcongomani huyo amesema kwa mujibu wa kanuni, ana uhakika kuwa atalipwa mara mbili ya pesa anazodai kutokana na usumbufu aliopata
Ni dhahiri Zahera hakufurahishwa na uamuzi wa uongozi wa Yanga kumfuta kazi, anachokifanya sasa ni kama 'kukomoa' pamoja na kuwa madai hayo ni stahiki yake na lazima alipwe
Hata hivyo Zahera anaifahamu hali ya kiuchumi ya Yanga, ndio maana wakati akiwa kocha wakati mwingine alilazimika kutumia fedha zake
Lakini uamuzi wa kwenda kushitaki FIFA ni dhahiri una lengo la kukomoa
Uongozi wa Yanga utalazimika kufanya jitihada za kumlipa haraka kwani kadiri watakavyochelewa ndivyo madai hayo yataendelea kuongezeka