Mshambuliaji David Molinga ndiye mchezaji aliyezungumzwa zaidi na mashabiki wa Yanga baada ya mchezo dhidi ya Biashara United jana
Ni mchezo ambao mshambuliaji huyo alicheza chini ya kiwango, alifanya matukio mengi ambayo hayakuwa na msaada kwa timu
Pengine ni wakati ambao Molinga anapaswa kujitathmini hasa baada ya Yanga kusajili washambuliaji wengine watatu
Baada ya kuwasajili Tariq Seif na Ditram Nchimbi, jana Yanga imempa mkataba wa miaka miwili mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Yikpe Gnamien
Gnamien aliyetua kutoka klabu ya Gor Mahia, alikabidhiwa jezi namba tisa

Molinga alijihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza baada ya Sadney Urikhob na Juma Balinya kushindwa kuonyesha ubora
Ukweli ni kwamba baada ya kuondoka wachezaji hao, Yanga haikuwa na mshambuliaji zaidi ya Molinga
Lakini kwa sasa hali ni tofauti, ushindani utakuwa mkubwa
Tariq jana alianza kwa kufunga bao katika mchezo wake wa kwanza
Bado Nchimbi na Yikpe hawajapata nafasi, lakini pasipo shaka watakuwa na shauku ya kufanya zaidi ili kujihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza
Ujio wa nyota hao unapaswa kuwa chachu ya kumfanya Molinga kuwa bora zaidi, athibitishe kile kilichosemwa na Mwinyi Zahera kuwa anao uwezo wa kufunga mabao 15 mpaka 20 kwenye ligi
Lakini kama sivyo ajiandae kukalia benchi na mwishoni mwa msimu akarejea kunako klabu yake
Kwani Molinga alitua Yanga kwa mkopo wa mwaka mmoja lakini mabingwa hao wa kihistoria waliahidi kuwa watamsajili moja kwa moja kama wataridhika nae