Pamoja na usajili wa Adeyum Saleh, kiraka Jaffar Mohammed ameonekana kumshawishi kocha Mkuu wa Yanga Luc Eymael ambaye amemtumia katika michezo miwili iliyopita dhidi ya Azam Fc na Singida United
Kabla ya Eymael kutua, Adeyum aliyesajiliwa dirisha dogo, alianza kujimilikisha nafasi ya beki wa kushoto wakati wa Kaimu kocha mkuu Charles Mkwasa
Jaffar ameonekana kucheza vizuri michezo miwili iliyopita, sasa anahusika sana pale timu inaposhambulia na pia kurudi kwa haraka kuzuia timu inapojilinda
Mchezaji mwingine ambaye amenufaika na ujio wa Eymael ni kiraka Said Juma Makapu

Katika mchezo uliopita dhidi ya Singida United Makapu alitumika kama mlinzi wa kati, akicheza sambamba na Lamine Moro
Alikuwa mmoja wa wachezaji waliocheza vizuri sana, aliwanyamazisha wale waliokuwa wakikosoa kuanzishwa kwake kwenye kikosi cha kwanza baada ya mkongwe Kelvin Yondani, Ally Mtoni na Andrew Vicent wote kukosekana
Hata kwenye mchezo dhidi ya Azam Fc, Makapu aliingia katika kipindi cha pili
Kiwango cha Makapu ambaye yuko Yanga kwa msimu wa tano kimeendelea kuimarika na hakuna shaka, uwezo wake wa kucheza namba zaidi ya moja utampa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha Eymael