Uongozi wa klabu ya Yanga umetangaza kukosa imani na Bodi ya Ligi kutokana na matukio mfululizo ya uonevu wanayofanyiwa na Bodi hiyo
Aidha kitendo cha Bodi hiyo kukiri kuisahau kuipangia Yanga mchezo wa ligi kuu katikati ya wiki, kinadhihirisha ukweli malalamiko ya mda mrefu ambayo Yanga imekuwa ikitoa kwa Bodi hiyo
Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalenela amesema hawana imani na Bodi hiyo na sasa wanaangalia utaratibu wa kupeleka malalamiko yao vyombo vya juu vya usimamizi wa soka nchini pengine hata kupeleka malalamiko FIFA
"Wenzetu wanacheza kila siku sisi hatuchezi, tukiwaandikia barua kuhoji hawatujibu. Sisi tumecheza mechi chache kuliko timu zote lakini bado hatupangiwi mechi zetu, halafu wanatoka kwenye vyombo vya habari wanasema wametusahau, hili haliingii akilini"
"Tumekata tamaa kuzungumza nao kwani wameonyesha dhahiri hawana nia njema na timu yetu. Tunaangalia jinsi ya kupata suluhisho kutoka vyombo vya juu," amesema
Juzi Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Steven Mguto alijitokeza hadharani kuomba radhi uongozi wa Yanga baada ya kuwasahau kuwapangia mchezo katikati ya wiki
Hata hivyo kitendo hicho kimewashangaza wadau wengi wa soka nchini na kuibua maswali miongoni mwao
Pengine hilo linaweza kuwa tukio la kwanza duniani kwa timu kusahauliwa kupangiwa ratiba ya kucheza mechi wakati ligi inaendelea
Aidha baadhi wanaamini tukio hilo halikufanyika kwa bahati mbaya kwani ukweli unaweza kuonekana kwenye ratiba iliyotolewa na Bodi hiyo kwa mechi ambazo Yanga itacheza mwezi wa pili
Watalazimika kucheza mechi tisa katika kipindi cha siku 29 ikiwa ni wastani wa kushuka dimbani kila baada ya siku tatu