Msimu uliopita Mwinyi Zahera alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga. Ni kutokana na kazi kubwa aliyokuwa akiifanya wakati ambao timu ilikuwa na matatizo lukuki
Hata hivyo mambo yalikuja kubadilika mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuondoshwa kwenye michuano ya kombe la Shirikisho kwa kufungwa jumla ya mabao 5-1 na Pyramids Fc katika michezo miwili
Zahera bado yuko nchini akiendelea na maisha yake, mwenyewe amesema amechagua kuishi Tanzania kwa kuwa ni nchi yenye amani na utulivu
Aidha Mcongomani huyo yuko mbioni kufungua kituo cha kulelea watoto wenye vipaji yaani 'Academy'
Juzi tulipata nafasi ya kuzungumza nae mambo machache kuhusu mtazamo wake kwa kikosi cha Yanga cha sasa ukilinganisha na kile chake
Uchezaji
Wakati huu Yanga inaonekana kuwa bora zaidi chini ya kocha Luc Eymael, wamekuwa wakitandaza soka la kitabuni, tofauti na wakati wa Zahera lakini mwenyewe amelizungumzia hilo
"Unajua kila kocha ana falsafa yake. Mimi nilikuwa na mfumo wangu ambao niliutumia msimu mzima uliopita na kufanikiwa kumaliza nafasi ya pili ligi kuu. Kocha wa sasa nae ana mfumo wake hivyo mabadiliko ya kiuchezaji ni jambo la kawaida", alisema Zahera
"Lakini pia wachezaji wanacheza katika vipindi tofauti. Sasa wanacheza wakiwa na uhakika wa maisha yao, wanalipwa mishahara, posho na motisha kwenye kila mchezo"
"Wakati wangu mambo hayo hayakuwepo, wakati mwingine wachezaji hawakulipwa mishahara hadi miezi mitatu, walikuja mazoezini huku hawafahamu wakirudi nyumbani wanakula nini"
"Tulifanya kazi kubwa ya kuwahamasisha, walijitolea kwa nguvu zao zote na timu ikafanya vizuri"
Ubora wa kikosi
Baadhi ya nyota wapya ambao Zahera aliwasajili, wameachwa huku wengine wakikosa uhakika wa namba kwenye kikosi cha kwanza
"Ni utashi wa kocha kuwatumia wachezaji ambao wanakwenda sawa na mfumo wake. Msimu uliopita hatukuwa na kikosi imara hivyo tulipaswa kusajili wachezaji wapya"
"Wachezaji wote tuliowasajili tuliwahitaji na nakuhakikishia kama mpaka leo ningekuwa bado niko Yanga ungewaona wanafanya vizuri"
"Kabla ya kuwasajili tulijiridhisha na uwezo wao. Leo hii mchezaji kama Juma Balinya ameondoka Yanga kasajiliwa na Gor Mahia, mchezo wake wa kwanza kwenye ligi kafunga mabao mawili, huwezi kusema alikuwa mchezaji mbaya. Mashabiki hawakumpa nafasi ya kudhihirisha ubora wake"
"Sadney, Balinya wangefanya vizuri hapa kama ilivyo kwa Molinga ambaye pia mwanzoni mlimuona hafai"
Amsifu Morrison
Zahera ameeleza kuvutiwa na uchezaji wa Bernard Morrison aliyetua Yanga mwezi Januari
"Katika timu yangu nilikuwa na changamoto ya washambuliaji wa pembeni. Hili nililizungumza mara kwa mara nilipokutana na wanahabari. Morrison ni mfano wa aina ya wachezaji ambao hata mimi niliwahitaji"
"Ni mchezaji mwenye maamuzi sahihi, anajua kuutumia mpira kwa manufaa ya timu, msumbufu, hatabiriki, anawapa mabeki wakati mgumu"
Nafasi ya Yanga kuwa bingwa
Zahera amesema Yanga bado ina nafasi ya kuwania ubingwa msimu huu kwani mechi bado ni nyingi
"Nafasi ya kuwa mabingwa wanayo kama watafanya vizuri kwenye mechi zote zilizobaki. Simba wanaongoza, lakini hata Azam Fc ni timu nzuri hivyo washinde mechi zao lolote linawezekana"