Baada ya kuibuka tetesi kuwa klabu ya Simba inamnyemelea mshambuliaji Bernard Morrison, Yanga iko mbioni kumuongezea Mghana huyo mkataba wa muda mrefu
Morrison alitua Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo mwezi uliopita akitokea klabu ya DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Mshambuliaji huyo wa zamani klabu ya Orlando Pirates, ameonyesha uwezo mkubwa katika mechi tano alizocheza mpaka sasa
Amefunga mabao mawili na kutoa pasi tatu za mabao kwenye mashindano yote
Inaelezwa awali Yanga walimpa mkataba wa muda mfupi lakini baada ya kuridhishwa na kiwango chake, wameamua kuurefusha mkataba huo
Gazeti la Championi la leo limedai kuwa Simba wameanza jitihada za 'chinichini' kumshawishi mshambuliaji huyo ajiunge nao mwezi Juni
Lakini uongozi wa Yanga umeshtukia janjajanja hiyo na kuahidi kuchukua hatua haraka
"Morrison hawezi kujiunga na Simba, mchakato wa kumuongeza mkataba utakamilika muda sio mrefu. Ni mchezaji muhimu sana kwetu, hao wanaojaribu kufanya ujanja ujanja wanapoteza muda wao," alisema mmoja wa watu wa ndani ya uongozi wa Yanga
Kwa miaka ya hivi karibuni Simba imekuwa ikivuruga sana usajili unaofanywa na watani zao Yanga
Luis Miquissone na Shiza Kichuya waliosajiliwa na Simba dirisha dogo wote walikuwa kwenye mipango ya Yanga lakini Simba ikaingilia kati na kuwasajili licha ya kutokuwa na shida kwenye maeneo wanayocheza
Nyota hao ni kama wamesajiliwa ili kuikomoa Yanga kwani tangu wawasajili, wanaonekana kwa nadra sana dimbani
Hata hivyo GSM iliyosimamia usajili wa Yanga dirisha dogo, ikapindua mezi kibabe na kumuibua Morrison ambaye usajili wake ni pendekezo la kocha Luc Eymael
Sasa Simba inaonekana kumnyemelea Mghana huyo baada ya kubaini ni 'bonge' la mchezaji
Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Yanga Charles Mkwasa ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi wa timu hiyo, aliwahi kuponda mfumo wa usajili wa klabu ya Simba kuwa hawana vitengo vya kusaka wachezaji wenye vipaji na badala yake wanasubiri wale wanaowindwa na Yanga
Wakati akiwa Katibu Mkuu, Mkwasa aliibua utaratibu wa kusajilil kimya kimya ili kukwepa janja janja hiyo ya Simba