Kikosi cha Yanga jioni ya leo kitashuka kwenye uwanja wa Mkwakwani kuikabili Coastal Union katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali
Baada ya kulazimishwa sare katika michezo mitatu iliyopita, Yanga inahitaji matokeo ya ushindi leo
Hata hivyo inakutana na Coastal Union ambayo ina msimu mzuri ikifanya vizuri katika mechi zinazopigwa katika uwanja wao wa nyumbani
Wagosi hao wa kaya waliangukia pua mechi iliyopita wakichapwa mabao 2-1 na Ruvu Shooting kwenye mchezo ambao ulipigwa hapohapo mkwakwani
Hivyo nao wataingia kwenye mchezo huo wakiwa na shauku ya matokeo ya ushindi
Lakini pia kuna upinzani umejenga baina ya timu hizo kwa kile kinachoaminiwa kuwa Coastal Union ina mahusiano na klabu ya Simba
Yanga pia imepata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki wa African Sports, ambao ni wapinzani wakuu wa Coastal Union
Ukizama kwenye historia utafahamu kuwa African Sports ilianzishwa kupitia mgongo wa Yanga wakati Coastal Union imetokana na mgongo wa Simba
Mkufunzi wa Yanga Luc Eymael amesema wanatarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa Coastal Union lakini lengo lao ni kuhakikisha wanaondoka na alama zote tatu
Mchezo utapigwa kuanzia saa 10 Alasiri