Aina ya ushangiliaji aliotumia mshambuliaji Bernard Morrison baada ya kuwafunga Simba kwenye mchezo wa ligi kuu March 08, imeendelea kuwa gumzo
Kupitia kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii, watu mbalimbali wametumia staili hiyo kama sehemu ya burudani
Wengine wanaitumia kuingia katika ofisi zao huku mtaani kwa watoto ikiwa ni staili yao mpya ya ushangiliaji katika michezo
Morrison afunguka alikoitoa
Morrison amefichua kuwa staili hiyo hajaanza kuitumia akiwa Yanga bali amekuwa akitumia hata alipokuwa Afrika Kusini akiwa Orlando Pirates.
"Watu wasielewe vibaya hii ni staili yangu na binti yangu Lelo, ni hivi Lelo wakati akiwa na mdogo sana alikuwa akipenda kucheza tukiwa nyumbani akiinua mguu mmoja kama vile huku anacheka kama ananitania," alisema Morrison na kuongeza;
"Amekuwa akipenda sana kufanya hivyo hata akikuudhi anakufanyia hivyo sasa unajikuta wewe mwenyewe hata kama ulikasirika unacheka sasa na mimi kwa kuwa binti yangu anapenda nikaona kila ninapofunga niwe nafanya kama yeye (Lelo)."