Usajili wa mshambuliaji Yikpe Gnamien ni moja ya sajili ambazo hazikufurahiwa kabisa na mashabiki wa Yanga
Nyota huyo aliyetua dirisha dogo akiwa mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba wake na Gor Mahia, amejikuta akikosa imani kutoka kwa mashabiki wa mabingwa hao wa kihistoria
Yikpe alijiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili na mpaka sasa ameifungia timu hiyo mabao mawili
Nyota huyo raia wa Ivory Coast amekuwa akijifua kwelikweli wakati huu ambao ligi imesimama kutokana na janga la corona
"Ni jukumu langu kufanya mazoezi kuhakikisha nakuwa timamu muda wote. Naamini ligi itakaporejea nitakuwa tayari kuisaidia timu yangu"
"Nitahakikisha nafanya vizuri kwa kila nafasi nitakayopewa na Mwalimu. Najiamini, sikuja Yanga kwa bahati, mashabiki wawe na subira, watafurahi" amesema

Yikpe ni miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa wakipewa nafasi mara kwa mara na kocha Luc Eymael licha ya mashabiki kutokuwa na imani nae
Katika moja ya mahojiano yake, Eymael alisema nyota huyo anakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo alipaswa kuzirekebisha ili awe bora zaidi
Bila shaka atahitaji kutumia vyema nafasi kwenye mechi zilizobaki ili kuwapa viongozi wa Yanga sababu ya kuendelea kumbakisha Jangwani
Kwani kwa michakato inayoendelea sasa, huenda akawa miongoni mwa wachezaji watakaopewa mkono wa kwaheri mwishoni mwa msimu kama mambo hayatabadilika