Uongozi wa Azam FC, umewataka Yanga kufuata taratibu kama ambavyo ulifanya wakati ikiwapa baraka za kumsajili mshambuliaji wao, Ditram Nchimbi, ambaye kwa sasa anaitumikia miamba hiyo ya mtaa wa Twiga na Jangwani
Kauli hiyo imekuja baada ya kuibuka taarifa za Yanga kuhitaji saini ya kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye hivi karibuni ameongeza mkataba wa mwaka mmoja unaomfanya kuitumikia timu hiyo ya Chamazi jijini Dar es Salaam hadi mwaka 2021.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ alisema Sure Boy bado ana mkataba wa mwaka mmoja zaidi wa kukitumikia kikosi hicho, hivyo kama Yanga inamhitaji inakaribishwa mezani kufuata taratibu zote kama ambavyo ilifanya wakati walipohitaji huduma ya Nchimbi.
Alisema hawajakutana na wala kuwajafuatwa na klabu hiyo au timu yoyote ambayo inahitaji kufanya nao mazungumzo kwa lengo la kumsajili mchezaji huyo ama mwingine ndani ya kikosi cha timu yao.
“Sisi hatumzuii mchezaji yeyote kuondoka, ila Sure Boy ni mchezaji wa Azam, ana mkataba mrefu bado na sisi, kama Yanga inamhitaji ifuate taratibu walizofuata awali na kisha kutoa pesa kumnunua Nchimbi,” Popat alinukuliwa na gazeti la Nipashe
Alisema kawaida ilivyo kwa klabu ama timu ikihitaji mchezaji mwenye mkataba, inafanya mawasiliano na klabu inayommiliki kwa ajili ya makubaliano ya pande zote tatu; zikianza klabu kwa klabu na baadaye mchezaji ambaye atakuwa na uamuzi wa kukubalia ama kukataa.
Popat alisema hawawezi kuweka thamani ya nyota huyo kutokana na ukweli kwamba hakuna timu ambayo imeonyesha dhamira ya kumhitaji licha ya kuona na kusikia katika vyombo vya habari kuwa Yanga inahitaji huduma yake.