Mshambuliaji wa Namungo Fc Reliants Lusajo ambaye amekuwa akihusishwa kutakiwa na Yanga, amesema kama itatokea akasajiliwa na timu hiyo,ataendeleza makali aliyokuwa nayo sasa Namungo Fc
Lusajo anashika nafasi ya pili kwenye orodha ya vinara wa mabao ligi kuu ya Vodacom akifunga mabao 11 sawa na Yusuf Mhilu wa Kagera Sugar
Nyota hao wako nyuma ya Mnyarwanda Meddie Kagere aliyetupia mabao 19 akiwa na klabu yake ya Simba
Lusajo ambaye hakutaka kuweka wazi kuhusu ukweli wa tetesi zinazomuelekeza Jangwani akieleza kuwa sio wakati wake kulizungumza hilo, amesema tetesi hizo zinampa faraja na kuona kazi yake inaonekana uwanjani
Amesema kama atasajiliwa na Yanga, anaamini hakuna kitu kitamfanya ashindwe kuyafanya yale yote anayoyafanya sasa kunako klabu ya Namungo
"Ninaamini kwamba uwezo wa mchezaji huwa haujifichi, iwapo nitapata nafasi ya kusajiliwa Yanga, nitaendelea na kasi yangu ya kutupia pale nitakapopata nafasi
"Uzuri ni kwamba kwa sasa nimezidi kuimarika na kuwa na uwezo wa kufunga jambo ambalo linanifanya niamini kwamba ninaweza kucheza popote ndani na nje ya Tanzania," amesema
Nyota huyo msomi amekuwa akihusishwa kuwindwa vikali na mabingwa hao wa kihistoria ambao aliwahi kuwatumikia mwaka 2013 ikielezwa kocha Luc Eymael amempendekeza miongoni mwa wachezaji wazawa aliopanga kuwasajili
Msimu huu Yanga imekuwa na changamoto kubwa kwenye safu yake ya ushambuliaji
Mabosi wa Yanga wamejipanga kuhakikisha msimu ujao wanakuwa na safu bora zaidi ya ushambuliaji ambayo itawasaidia kwenye mbio za kuwania ubingwa ambao watakuwa wameupoteza kwa watani zao Simba kwa misimu mitatu mfululizo