Mlinda lango wa Yanga Metacha Mnata amesema moja ya ndoto zake ni kupata nafasi ya kwenda kusakata kabumbu nje ya nchi
Metacha ambaye kwa sasa amejihakikishia kuwa kipa namba moja wa kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria, amesema ni ndoto ya kila mchezaji kuona anapiga hatua kutoka pale alipo
"Suala la kwenda kucheza soka nje ya nchi huwa nalifikiria. Nadhani ni ndoto ya kila mchezaji, naendelea kujituma na kufanya mazoezi kwa bidii ili siku moja niweze kufanikiwa," amesema Metacha
Metacha alitua Yanga kutoka klabu ya Mbao Fc ambao alikuwa akiitumikia kwa mkopo kutoka Azam FC
Msimu wake wa kwanza na Yanga umekuwa mzuri na hata kuweza kujihakikishia nafasi kwenye kikosi cha kwanza mbele ya Mkenya Farouk Shikhalo ambaye Yanga ilimsajili kwa lengo la kumfanya awe kipa namba moja
Makali yake yalianza kuonekana kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika akipata nafasi kwenye michuano hiyo kufuatia kibali cha Shikhalo kuchelewa
Alitoa mchango mkubwa kuivusha Yanga kwenye raundi ya kwanza ugenini kule Botswana ambako Yanga ilifanikiwa kushinda bao 1-0 dhidi ya Township Rollers
Katika mchezo huo Metacha aliokoa mkwaju wa penati