Afisa Mhamasishaji wa Yanga Antonio Nugaz amewataka wapenzi, wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kuwa na amani kwani wamejipanga kurejesha heshima ya timu hiyo msimu ujao
Tangu kurejea kwa GSM, tetesi za usajili kuhusu nyota mbalimbali wanaohusishwa na Yanga zimeendelea kuongezeka
Juzi zilizagaa tetesi kuwa GSM wako mbioni kuwanasa wachezaji wawili wa Simba kiungo Clatous Chama na winga Deo Kanda
Akizungumzia tetesi hizo Nugaz amesema hawana masihara katika usajili wa awamu hii. Amesema nyota yeyote atakayependekezwa na kocha Luc Eymael watamsajili
"Ngoja nikwambie rafiki yangu, hakuna mchezaji yeyote wa ndani ambaye kocha wetu atampendekeza tutashindwa kumsajili. Hao wa nje, kama dau lake ni chini ya dola laki tano tutamsajili"
"Hivyo kigezo chetu ni mapendekezo ya kocha, kama wachezaji hao Eymael anawataka tutawasajili. Na sio hao tu hata akipendekeza timu nzima, tutaisajili," alitamba Nugaz
Mpaka sasa Yanga kupitia wadhamini wao GSM wamefanikiwa kuwaongezea mikataba nyota wao muhimu Papy Tshishimbi na Bernard Morrison huku wakiendelea na mazungumzo kuhuisha mikataba ya nyota wengine
Lakini Nugaz ametamba kuwa moto utawaka dirisha la usajili litakapofunguliwa mwezi Juni