Kocha Mkuu wa Yanga Luc Eymael ameeleza kutokuwa na raha baada ya safari yake ya kurejea nchini kufutwa kutokana na janga la corona
Eymael ambaye alikuwa na tiketi yake mkononi kuanza safari kurejea jijini Dar es salaam kesho Jumatano, amesema kuendelea kuchelewa kurudi nchini kunamvurugia mipango yake
Juzi Mamlaka ya Usalama ya Anga Tanzania (TCAA) ilitangaza kufuta safari zote za ndege za abiria za Kimataifa baada ya kasi ya maambukizi ya virusi vya corona kuongezeka nchini
Mbelgiji huyo atalazimika kuendelea kubaki huko kwao kusubiri maelekezo ya Serikali ya Tanzania kutegemea na mwenendo wa maambukizi ya virusi vya COVID-19
"Nilikuwa na tiketi mkononi lakini nimeshindwa kusafiri kutokana na changamoto hii ya corona"
"Sijafahamu ni lini safari za ndege zitaruhusiwa... nakosa raha kwani kulikuwa na mikakati nimeiandaa kuifanya nitakaporejea Tanzania. Kuna mambo mengi ya manufaa kwa klabu yangu ningeyafanya licha ya ligi kuwa imesimama," amesema
Eymael alipewa ruhusa ya kwenda kwao Ubelgiji kufunga ndoa ambayo aliifanya March 27 2020