Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela ameuomba radhi uongozi wa Simba kwa kile alichoeleza kuwa hakuna mazungumzo yoyoye ambayo uongozi wa Yanga umefanya na kiungo wa timu hiyo Clatous Chama
Mwakalebela jana alieleza klabu ya Yanga kuwa kwenye mchakato wa kumsajili Chama, amesema alichokuwa akifanya yeye ni utani kama ambavyo Simba walikuwa wakifanya kwa kiungo Papy Tshishimbi
"Nichukue nafasi hii kuwaomba msamaha Simba Sports Club na wanachama wa Yanga SC kuhusu kauli yangu juu ya kutaka kumsajili Claotous Chama"
"Nilikuwa nafanya utani kama wao walivyokuwa wanafanya kwa Tshishimbi ila kiukweli mchezaji huyo sijazungumza nae. Nilizidisha utani na naahidi jambo hili halitojitokeza tena," amesema
"Utaratibu kuhusu masuala ya usajili tunayatambua vema ila nilichokifanya ilikuwa ni sehemu ya maisha ya utani, nimeona Ofisa Habari wao Haji Manara amezungumza, hili ni soka na kanuni zipo wazi,"
Mapema leo uongozi wa Simba kupitia kwa msemaji wao Haji Manara, ulidai kuwa wameandika barua kwa shirikisho la soka nchini (TFF) kupeleka malalamiko rasmi baada ya klabu ya Yanga kutangaza kumuwania mchezaji wao ambaye wamedai bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Simba