Kama itatokea ligi itarejea kabla ya kufunguliwa kwa mipaka ya nchi mbalimbali iliyofungwa kutokana na janga la corona, uongozi wa Yanga umesema timu itasimamiwa na kocha msaidizi Charles Mkwasa
Kocha Mkuu wa timu hiyo Luc Eymael ameshindwa kurejea baada ya Serikali ya Ubelgiji na hapa Tanzania kutangaza kusitisha safari za ndege kutoka nje ya nchi katika jitihada za kudhibiti COVID-19
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema kama kocha wao atashindwa kurejea kwa wakati na ligi ikawa imeanza, majukumu yake yatasimamiwa na Mkwasa
Hata hivyo jana Serikali imetangaza kuendelea kusitisha shughuli zote zenye mikusanyiko nchini mpaka pale itakapotangaza vinginevyo
Kulingana na taarifa ya Waziri Mkuu, mpaka kufikia jana, idadi ya wagonjwa walioambukizwa corona nchini Tanzania ni 53
Serikali imewasisitizia Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo kwa kufuata maelekezo yanayotolewa