Hakuna ubishi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela aliteleza kwa kuzizungumza hadharani tetesi za usajili unaomhusu kiungo wa Simba Clatous Chama licha ya kuwa mwenyewe amesema ulikuwa utani
Masuala haya ya usajili yana mitego mikubwa, ndio maana popote duniani huwezi kumsikia kiongozi wa klabu flani akisema tunataka kumsajili mchezaji wa timu nyingine kama hakuna mchakato unaoendelea baina ya timu hizo
Nakumbuka miaka michache iliyopita, Yanga na Simba ziliingia kwenye mvutano wa usajili wa beki wa kulia Hassan Kessy ambaye alitoka Simba kujiunga na Yanga
Kessy alikuwa akisubiri mkataba wake na Simba umalizike ili ajiunge na Yanga lakini katika moja ya mechi za Yanga, alionekana uwanjani ambapo alionekana akikabidhiwa uzi wa Yanga na mmoja wa viongozi wa timu hiyo
Tukio hili lilipelekea Yanga kulazimika kulipa Tsh Milioni 50, fedha ambazo aliyekuwa Mwenyekiti wakati huo Yusufu Manji alizilipa
Viongozi hawapaswi kujiingiza kwenye haya masuala ya tetesi ni vyema wakayaacha kwa mashabiki
Kiongozi ni vyema akajitokeza hadharani pale tu anapokuwa na uhakika na jambo analozungumza
Inafahamika Yanga, Simba pamoja na vilabu vingi tu duniani, vimekuwa vikifanya michakato ya usajili nyuma ya pazia nje ya utaratibu unaoruhusiwa na FIFA lakini mambo haya huwa hayazungumzwi hadharani
Wenye nafasi ya kuzungumza michakato hii ni vyombo vya habari na mashabiki ambao hawabanwi na sheria yoyote
Ni vyema masuala haya wakaachiwa wao, viongozi wajiepushe kujiingiza kwenye mitego ambayo inaweza kuwaingiza matatani