Inaelezwa Yanga tayari imeshamalizana na mshambuliaji wake wa zamani Reliants Lusajo ambaye anaitumikia klabu ya Namungo Fc
Lusajo ndiye kinara wa mabao katika timu hiyo akiwa amefunga mabao 11, lakini pia anashika nafasi ya pili katika vinara wa mabao ligi kuu ya Vodacom msimu huu akiwa sawa na Yusuph Mhilu wa Kagera Sugar
Hivi karibuni nyota huyo aligoma kuongeza mkataba, hali iliyopelekea uongozi wa timu hiyo kukiri kuwa wanaweza wasiwe nae msimu ujao
Inaelezwa mpango wa Yanga ni kumsajili yeye pamoja na mpishi wa mabao yake Lucas Kikoti ambaye msimu huu amefunga mabao manne na kutoa pasi sita za mabao
Hata hivyo Kikoti bado ana mkataba wa mwaka mmoja zaidi na klabu ya Namungo hivyo mabingwa hao wa kihistoria kuweza kuipata saini yake, ni lazima wamalizane na Namungo Fc kwanza, jambo ambalo linaonekana kuwa gumu
Namungo Fc inalelewa na Mbunge wa Jimbo wa Ruangwa ambaye ni Waziri Mkuu wa Tanzania Mh Kassim Majaliwa
Kumekuwa na tetesi kuwa Kikoti pia anawaniwa na Simba ambayo Makao Makuu yake ni Mtaa wa Msimbazi
Yanga ina mkakati kabambe wa kuisuka upya safu yake ya ushambuliaji ambayo msimu huu imeshindwa kufurukuta
Inaelezwa katika nafasi ya mshambuliaji wa kati, ni Ditram Nchimbi pekee ambaye amejihakikishia kuendelea kubaki Jangwani msimu ujao
David Molinga, Yikpe Gnamien na Tariq Seif majaliwa yao yako mikononi mwa kocha Luc Eymael