Zipo taarifa kuwa miongoni mwa nafasi ambazo kocha Luc Eymael amependekeza usajili mpya ni nafasi ya mlinda lango
Kwa sasa Yanga ina walinda lango watatu, Metacha Mnata, Farouk Shikhalo na Ramadhani Kabwili
Farouk na Metacha ndio wamepata nafasi zaidi msimu huu wakati Kabwili hakupata nafasi ya kucheza mechi yoyote ya kimashindano
Lakini msimu uliopita Kabwili ndio alikuwa kipa tegemeo hasa baada ya Beno kufanya mgomo
Pengine msimu huu hakupata nafasi ya kudhihirisha ubora wake, Yanga inaweza kufanya makosa kama wataamua kumuacha
Kabwili umri wake bado ni mdogo, ana muda mrefu wa kusakata kabumbu
Alijiunga na Yanga akiwa na umri wa miaka 17 tu na ameingia kwenye rekodi ya CAF ya mchezaji mdogo zaidi kucheza michuano ya ligi ya mabingwa Afrika, akidaka mchezo dhidi ya Township Rollers mwaka juzi
Kabwili bado ni miongoni mwa makipa bora Tanzania, changamoto ya kukosa nafasi ndio inamfanya asionekane
Pengine ligi itakaporejea, kwenye mechi zilizobaki ni vyema mlinda lango huyo akapewa nafasi ya kukaa langoni katika mechi kadhaa
Naamini kama Eymael atamshuhudia Kabwili katika mechi tatu tu, atafuta mpango wake wa kusaka mlinda lango mwingine