Kocha Msaidizi wa Yanga Charles Mkwasa amelipongeza Shirikisho la soka duniani (FIFA) kwa kuja na pendekezo la kuongeza idadi ya wachezaji wa akiba wanaoweza kutumika kwenye mchezo mmoja kutoka watatu mpaka watano
Mkwasa amesema uamuzi huo utawapa makocha wigo mpana wa kuimarisha timu zao wakati wa mchezo
Hata hivyo ametahadharisha kuwa wingi wa 'sub' hizo unaweza kuwa na athari kwa uchezaji wa timu
"Ni mpango mzuri kwani makocha watakuwa na nafasi ya kuboresha na kuongezea nguvu timu zao wakati mchezo ukiendelea lakini ni muhimu kwao kuwa makini kwani idadi kubwa ya mabadiliko inaweza kuwa na athari kwa mwenendo wa uchezaji wa timu," amesema
FIFA imetoa mapendekezo hayo yatumike wakati ligi zitakaporejea baada ya udhibiti wa janga la corona
Ni kutokana na changamoto itakayojitokeza ambapo mechi nyingi zitapaswa kupigwa ndani ya muda mfupi huku wachezaji wakiwa wamekaa bila ya kucheza kwa muda mrefu
Uamuzi huo unatajwa kuwa na lengo la kulinda afya za wachezaji