Mshambuliaji wa zamani wa Yanga Heritier Makambo jina lake linatajwa sana kuwa huenda msimu ujao akarejea nchini kuvaa uzi wa njano na kijani kwa mara ya pili
Makambo ambaye Yanga ilimuuza klabu ya Horoya AC baada ya msimu mmoja wa mafanikio, amerejea kwao DR Congo wakati huu ambao ligi zimesimama kutokana na janga la corona
Aidha tayari Guinea imetangaza kufuta msimu kutokana na janga hilo hivyo mwamba huyo anaweza asirejee tena Horoya Ac kama Yanga kupitia moja ya wadhamini wao, GSM watafanikiwa kuipata saini yake
Katika moja ya mahojiano yake aliyofanya na chombo kimoja cha habari nchini, Makambo alieleza kukumbuka shamra shamra za soka la Tanzania
"Nimewakumbuka mashabiki wa soka Tanzania hasa mashabiki wa Yanga vile jinsi wanavyoingia uwanjani kwa wingi kushangilia timu yao. Mashabiki wa Tanzania wanapenda sana mpira kuliko Guinea," alisema
Makambo alisema kuwa amewakumbuka nyota wote wa kikosi cha Yanga aliocheza nao msimu uliopita akimtaja Papy Tshishimbi kuwa ndiye aliyekuwa mtu wake wa karibu zaidi kwa kuwa ndiye aliyemfundisha mambo mengi Tanzania
"Wachezaji wote wa Yanga walikuwa rafiki zangu lakini Tshishimbi ilikuwa zaidi kwa sababu wakati nilipokuja Tanzania yeye ndiye aliyenifundisha kila kitu inayohusu Yanga"
Aidha Mzee huyo wa kuwajaza, amesema kama atarejea nchini atatamani kucheza na wchezaji kama Tshishimbi, Ajib, Paulo Godfrey, Fei Toto na nyota wengine wa Yanga
Makambo amemtaja Ajib kama mchezaji aliyechangia mabao mengi aliyofunga wakati yuko Yanga
Hata hivyo kwa sasa Ajib ametimkia klabu ya Simba na ikitokea Makambo akarejea nchini, hatamkuta kinara huyo wa 'assist' msimu uliopita
Lakini atawakuta mafundi wengine kina Bernard Morrison, Mapinduzi Balama, Haruna Niyonzima na mastaa kibao ambao wanaweza kuyafanya maisha yake ya kuzifumania nyavu kuwa rahisi