Kuna watu wanaweza kudhani ahadi wanazotoa GSM kuhusu usajili wanaokusudia kuufanya Yanga, ni siasa za mpira tu kama ilivyozoeleka hapa nchini
Kwa hakika GSM watafanya jambo kubwa dirisha la usajili litakapofunguliwa kwa kufanya usajili mkubwa ambao utakiboresha kikosi cha Yanga lakini muhimu zaidi kutengeneza mazingira mazuri ya mauzo ya jezi na bidhaa nyingine za klabu ya Yanga
Hivi karibuni GSM walisaini mkataba mwingine na klabu ya Yanga ambao utawawezesha kutumia nembo ya Yanga kutengeneza bidhaa nyengine zaidi ya jezi
Kwa mtazamo wa kibiashara, ubora wa timu utaifanya biashara yao pia ishamiri wakipata uzoefu kupitia usajili wa kiungo mshambuliaji Bernard Morrison
Katika kipindi cha muda mfupi, Morrison ameweza kuchagiza biashara ya mauzo ya jezi ambao hivi karibuni Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Mhandisi Hersi Said alikiri kuwa pamoja na changamoto ndogondogo zilizopo, wamenufaika na mauzo ya jezi za Yanga
Morrison aliyetua Yanga mwezi Januari ndiye anayeshilia rekodi kwa jezi yake namba 33 kununuliwa sana na mashabiki
Inaelezwa kuelekea mchezo dhidi ya Simba uliopigwa March 08, GSM walitengeneza jezi maalum za Morrison ambazo zilikuwa zikiuzwa Tsh 50,000/-
Nakala zaidi ya 5,000/- ziliuzwa na kuwaingia GSM zaidi ya Tsh Milioni 250,000/-
Barani ulaya ni kawaida vilabu kujitosa kununua wachezaji kwa bei ghali lakini wanakuwa na uhakika wa kurejesha fedha walizotumia wakati mwingine kupitia mauzo ya jezi tu
Mfano mzuri ni klabu ya Juventus ilipomnunua Cristiano Ronaldo kutoka Real Madrid. Miamba hao wa soka la Italia walirejesha fedha yao kupitia mauzo ya jezi katika kipindi kisichozidi siku 10 tu
Timu za Tanzania hazikuwa zikiiona fursa hii na pengine ndio sababu haziko tayari kununua wachezaji ghali kwa kuwa hakuna utaratibu mzuri wa kurudisha fedha hizo zaidi ya kutegemea mashabiki wanaoingia viwanjani
Lakini usajili ujao Yanga kupitia GSM wamekusudia kufanya usajili wa kisasa
GSM wameahidi kutumia fedha kusajili wachezaji bora huku iwakitenga zaidi ya Tsh Bilioni 1.5 kwa ajili ya zoezi hilo
Juzi Mhandisi Hersi Said aliwataka mashabiki wa Yanga wakae tayari kupokea majembe mapya yatakayoitumikia Yanga msimu ujao
Lakini kubwa zaidi, amedokeza kutakuwa na usajili ambao utatikisa nchi