Inaelezwa Yanga iko karibu kukamilisha usajili wa beki wa Coastal Union na timu ya Taifa Bakari Nondo Mwamnyeto
Mwishoni mwa wiki hii uongozi wa Coastal Union unatarajiwa kukutana na wenzao wa Yanga pamoja na wadhamini/wahisani wao GSM ili kukamilisha mazungumzo
Tangu mwezi Januari wakati wa dirisha dogo, Mwamnyeto beki kinda mwenye umri wa miaka 22, ametawala kurasa za michezo za vyombo vya habari baada ya kuzigonganisha Yanga na Simba ambazo zote zilikuwa zikimuwania
Taarifa za ndani ya uongozi wa Coastal Union zimebainisha kuwa Yanga inaelekea kushinda mbio za kuwania saini ya mlinzi huyo anayetabiriwa kuja kurithi mikoba ya mkongwe Kelvin Yondani
Ni Yondani mwenyewe aliyependekeza kwa uongozi wa Yanga kuwa wanapaswa kumpata mlinzi huyo kwa gharama yoyote
Yanga inaonekana kupania kuimarisha safu yake ya ulinzi ambayo msimu huu haikuwa kwenye ubora unaostahili ikiwa imeruhusu mabao 20 kwenye ligi
Mabingwa hao wa kihistoria pia wako mbioni kumuongeza mkataba beki wao kisiki Lamine Moro