Kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima amesema Tanzania itafanya makosa kama ilivyofanya nchi ya Rwanda wakipunguza idadi ya nyota wa kigeni
Niyonzima amesema Rwanda ilipunguza idadi ya wachezaji wa kigeni, hatua hiyo iliathiri maendeleo ya vilabu vyao vikubwa Rayon Sports na APR
"Miaka ya nyuma Rayon Sports na APR zilikuwa timu zenye ushindani mkubwa na zilikuwa zikiogopewa. Lakini tangu kupunguza wachezaji wa kigeni, ushindani umepungua sana," amesema Niyonzima
Aidha nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Rwanda amesema uwepo wa wachezaji wengi wa kigeni unawapa motisha wachezaji wazawa kujituma ili nao wapate nafasi kwenda kucheza nchi nyingine
"Mimi leo nacheza Tanzania, nilipokuwa Rwanda nilihamasishwa na wachezaji kutoka nje ya nchi. Nikaweka juhudi ili nami niweze kupata nafasi ya kutoka Rwanda"
Baada ya kukaa Tanzania kwa muda mrefu, Niyonzima amesema kwa sasa anachukulia Tanzania kama ni nyumbani kwake baada ya Rwanda
"Kama Tanzania ingekuwa inaruhusu uraia wa nchi mbili, ningechukua. Nafurahia maisha ya Tanzania, watoto wangu wamezaliwa hapa hivyo naona hapa ni nyumbani kwetu pia"