Mlinda lango wa KMC Jonathan Nahimana amedai kuwa alifuatwa na viongozi wa Yanga wakihitaji huduma yake pale Jangwani
Nahimana ambaye ni kipa namba moja wa timu ya Taifa ya Burundi, amebainisha hayo wakati akifanya mahojiano na redio moja maarufu nchini
Inaelezwa nafasi ya mlinda lango ni miongoni mwa maeneo yaliyopendekezwa na kocha wa Yanga Luc Eymael kuongezewa nguvu
Yanga ina walinda lango watatu Metacha Mnata, Farouq Shikhalo na Ramadhani Kabwili
Mpaka msimu unasimamishwa, Metacha na Shikhalo ndio waliopata nafasi zaidi ya kukaa langoni
Baadhi ya wadau wa mabingwa hao wa kihistoria hawaamini kama timu yao inahitaji mlinda lango mpya
"Yanga haina tatizo kubwa eneo la golikipa. Tunahitaji kuweka mkazo eneo la washambuliaji na ulinzi. Siungi mkono timu kusajili kipa mwingine tena wa kigeni. Hapa nchini tunao makipa wazuri tu, tena ingekuwa vyema iyo nafasi moja ya kipa tumtafute mzawa halafu tuitumie kusajili mchezaji wa ndani," amesema Rashid mdau wa Mwana Jangwani
Miaka ya karibuni Yanga imekuwa na utamaduni wa kusajili makipa wa kigeni licha ya kuwa baadhi yao walishindwa kufikia matarajio ya wengi
Misimu miwili iliyopita walikuwa na Mcameroon Youthe Rostand ambaye hata hivyo mkataba wake ulivunjwa wakamsajili Claus Kindoki ambaye pia alidumu kwa msimu mmoja tu Yanga
Baada ya Kindoki kuondoka, sasa Yanga wakamleta Mkenya Farouk Shikhalo ambaye pia pamoja na kuanza majukumu yake vyema mwanzoni wa msimu, sasa ameonekana kupoteza nafasi mbele ya mzawa Metacha Mnata
Wengi wanajiuliza, bado Yanga inahitaji kuwekeza kwenye makipa wa kigeni?