Baadhi ya wachezaji wa klabu ya Yanga wamejipanga kutumia vyema nafasi ya mechi zilizobaki ili kulishawishi benchi la ufundi
Baada ya Uongozi wa Yanga kwa kushirikiana na wadhamini wao GSM kuwa wamejipanga kukisuka upya kikosi chao, vita itakuwa kubwa sana kwenye mechi za mwisho kwani kila mchezaji atahitaji kufanya vizuri ili kulishawishi benchi la ufundi
Wakati Yanga ikiwa imeanza rasmi mchakato wa kufanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji, ni wazi wachezaji wanafahamu kuanzia msimu ujao maisha 'yatanoga' kwelikweli pale Mtaa wa Jangwani
Aidha kocha Luc Eymael alidokeza kuwa katika mechi zilizobaki hasa kwenye ligi, atawapa wachezaji wote nafasi kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho
Washambuliaji David Molinga na Yikpe Gnamien ni miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa na ratiba kali za mazoezi ili kujiweka sawa kabla ya ligi kurejea
Wakati Molinga akiahidi kuwa iwapo kocha atampa nafasi katika mechi zilizobaki, ana uhakika wa kufunga mabao kati ya saba na tisa, Yikpe amesema pamoja na kuanza maisha yake Yanga vibaya, anaamini hiyo itakuwa nafasi kwake kuwaonyesha mabosi wake kuwa hawakukosea kumpa mkataba wa miaka miwili
Bila shaka nyota hao wanaziona tetesi zinazowahusu washambuliaji mbalimbali wanaotajwa kuwaniwa na Yanga
Hivi karibuni Mkurugenzi wa Mashindano Yanga Thabiti Kandoro, alisema wamekuwa wakifuatilia ratiba za mazoezi ya wachezaji wote na wamejiridhisha kuwa nyota wao wako tayari kwa ngwe ya lala salama ligi kuu ya Vodacom