Msemaji na Mhamasishaji wa Yanga Antonio Nugaz amesema uongozi wa klabu hiyo umedhamiria kufanya mabadili sahihi ya mfumo wa uendeshaji, ndio sababu kwa kushirikiana na wadhamini wao GSM wamefuata Utaalamu Hispania kwa kampuni ya La Liga
Nugaz amesema anaamini mchakato huo utakamilishwa ndani ya muda uliopangwa na kuifanya Yanga kuwa klabu inayoendeshwa kisasa kama zilivyo timu kubwa kule Hispania
"Kila shabiki wa Yanga alitamani kuona siku moja timu yake inafanya mabadiliko ambayo yatakuwa na tija. Mwenyekiti Dk Msindo Msolla na timu yake ya uongozi, kwa kushirikiana na wadhamini wetu GSM ambao wamejitolea kusimamia mchakato mzima, wamekwenda Hispania kutuletea La Liga kampuni ambayo imetengeneza mifumo ya zaidi ya timu 40 kule Hispania"
"Tumedhamiria kufanya mabadiliko ya kweli ndio maana hatukutaka kuleta ujanja ujanja katika suala hili. kabla ya mwezi huu kukamilika, tutakuwa tumesaini mkataba na La Liga kuanza rasmi mchakato huo"
"Mchakato utakuwa na awamu tatu; awamu ya kwanza ambayo inaanza karibuni baada ya mkataba kusaini itachukua miezi sita, awamu ya pili na ya tatu zitachukua mwaka mmoja mmoja kulingana na mapendekezo yaliyotolewa na wataalamu"
"Kila Mwanayanga atembee kifua mbele, aunge mkono uongozi na tuwe pamoja kwenye mchakato huu ambao unakwenda kuifanya timu yetu ikaandike historia mpya," ametamba Nugaz
Mifumo ya timu za Hispania ikoje?
Ukifanya tathmini ya kina, utabaini uongozi wa Yanga pamoja na GSM, wamechukua uamuzi sahihi wa kufuata mifumo inaotumiwa na vilabu vya Hispania kwani kwa kiasi kikubwa inashabihiana na mfumo ambao Yanga imekuwa ikiutumia kwa miaka mingi
Kule vilabu vikubwa kama Fc Barcelona, Real Madrid, Atletico Madrid, Sevilla na hata Athletic Club, vinamilikiwa na Wanachama kwa asilimia 100
Vilabu hivi vinatengeneza pesa nyingi kupitia wadhamini, bidhaa za klabu, haki za matangazo ya televisheni pamoja na Wanachama na mashabiki wake
Mfano kwa klabu kama Fc Barcelona ina madaraja tofauti ya Wanachama ambayo unaweza kujiunga kulingana na uwezo wako
Kundi la Wanachama wa daraja la juu maarufu 'socio' ndio hupewa haki za kuwachagua viongozi wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ambayo juu yao kuna Rais
Aidha hata utaratibu wa kumpata huyu Rais ni tofauti, yapo masharti ambayo ni lazima mgombea akidhi ikiwemo kuwa Mwanachama wa klabu kwa kipindi kisichopungua miaka 30. Lakini pia lazima fedha iwepo...!
Hapohapo kwenye Uwanachama, klabu ina madaraja ya Wanachama kufuatana na umri. Mwanao mdogo unaweza kumkatia uanachama na akanufaika na fursa zote zinazotolewa kwa Wanachama kulingana na madaraja yao
Pia klabu inakuwa na vitengo ambavyo hujitegemea katika uendeshaji wake pamoja na kuwa viko chini ya Bodi ya Wakurugenzi
Kila kitengo kinawajibika kubuni miradi ambayo itaongeza mapato kwa klabu kwa maana timu itakuwa na mlengo wa kibiashara zaidi
Pamoja na kuwa mazingira yetu ni tofauti na kule Hispania, lakini ni wazi taswira ya kile ambacho La Liga wanakwenda kukifanya kwa Yanga, hakitatofautiana sana na muundo wa vilabu vingi kule Hispania
Mfumo mpya utakwenda kuifanya Yanga kuwa klabu yenye mvuto mkubwa wa kibiashara na hivyo kuvutia Wafanyabiashara wengi kuwekeza fedha zao