Mlinda lango wa Yanga Farouk Shikhalo huenda atachelewa kujiunga na wenzake kutokana na Serikali ya Kenya kuwa bado imefunga mipaka kutokana na janga la corona
Wachezaji wa Yanga walifanyiwa vipimo vya Afya juzi na jana wakaanza mazoezi huku nyota huyo akikosekana sambamba na kocha mkuu Luc Eymael ambaye hata hivyo anaweza kuwasili wiki ijayo
Uongozi wa Yanga umesema unafuatilia taratibu za kumrejesha nchini mlinda lango huyo
Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema pamoja na kuwa suala lake liko nje ya uwezo wao, wanapambana kuhakikisha anarejea nchini kwa wakati ili aungane na wenzake
"Suala la Shikalo lipo nje ya uwezo wetu, ila tunapambana kuhakikisha mchezaji huyo anarejea kwa wakati na kuwahi kabla ya ligi haijaanza rasmi," amesema Mwakalebela
Kwa sasa Yanga itamtegemea mlinda lango, Metacha Mnata huku wakati Ramadhani Kabwili akirejea taratibu baada ya kupona jeraha la kushonwa nyuzi nane kufuatia ajali ya pikipiki