Huko Jangwani mambo ni 'mswano' kwani baada ya kipindi cha machozi, jasho na damu, upepo mwanana umeanza kuvuma
Mwishoni mwa wiki Yanga ilisaini mkataba uliofungua rasmi mchakato wa mabadiliko mfumo wa uendeshaji unaosimamiwa na La Liga
Lakini pia, mabingwa hao wa kihistoria waliingia makubaliano ya ushirikiano na klabu ya Sevilla ikiwa ni ndani ya makubaliano ya mkataba wa La Liga
Wakati msimu huu ukielekea ukingoni, fununu za nyota ambao watasajiliwa kuwatumikia mabingwa hao wa kihistoria msimu ujao, zimeanza kutolewa
Mapema leo Mkurugenzi wa uwekezaji GSM, Mhandisi Hersi Said, alisema katika mkakati wao wa kusuka safu ya ushambuliaji, wamepania kushusha washambuliaji ambao waliibuka wafungaji bora katika ligi tano bora barani Afrika
Hivi karibuni CAF ilitaja orodha ya ligi kuu bora barani Afrika ambapo Ligi Kuu ya Tunisia ilishika namba moja, zikafuata ligi za Morocco, Misri, Algeria na DR Congo zikiwa ndio ligi tano bora
Ni katika ligi hizo washambuliaji wapya wa Yanga wanatarajiwa kusajiliwa kulingana na kauli ya Injinia Hersi Said
Hebu tuwaangalie vinara wa mabao katika ligi hizo
Mohammed Lamine Abid wa CS Constantine ndiye kinara wa mabao ligi kuu ya Algeria akiwa amefunga mabao 10 mpaka wakati ligi inasimama kutokana na corona
Anthony Okpotu yeye ndiye kinara wa mabao ligi kuu ya Tunisia, akiwa ameifungia US Monastir mabao 11
Abdallah Es Said wa Pyramids anaongoza pale ligi kuu ya Misri akiwa ametupia mabao 12
Pale Morocco kinara wa mabao wa ligi hiyo ni Reda El Hajhouj wa OCK Khouribga akiwa amefunga mabao 10
Pale DR Congo kuna Jackson Muleka wa TP Mazembe aliyefunga mabao 12 lakini pia amefungana na Mpiana Monzizi wa FC Lupopo aliyepachika mabao 12
Mpiana amekuwa akijwa zaidi kuwaniwa na mabingwa hao wa kihistoria, kwa nyakart tofuati mwenyewe alithibitisha 'kuchonga' na mabosi wa GSM
Je ni yeye? tusubiri...
Lakini pia Injinia Hersi alifichua kuwa watasajili winga matata kutoka miongoni mwa vilabu vinavyoshiriki ligi hizo tano bora Afrika
Orodha ya ligi 10 bora Afrika
1.Ligi kuu ya Tunisia.
2.Ligi kuu ya Morocco.
3.Ligi kuu ya Misri.
4.Ligi kuu ya Algeria.
5.Ligi kuu ya DR Congo.
6.Ligi kuu ya Afrika Kusini.
7.Ligi kuu ya Zambia.
8.Ligi kuu ya Sudani.
9.Ligi kuu ya Nigeria.
10.Ligi Kuu ya Guinea.