Tangu wiki iliyopita mlinzi Ali Hamad Ali na kiungo Raphael Daudi Lothi wanashiriki mazoezi ya kikosi cha Yanga kinachojiandaa na mechi za kumalizia msimu ligi kuu ya Vodacom pamoja na michuano ya kombe la FA
Nyota hao waliingia katika sintofahamu na uongozi wa Yanga mwezi Januari baada ya kugomea kutolewa kwa mkopo
Lothi alipaswa kujiunga na Singida United wakati Ali Ali alipelekwa klabu ya JKT Tanzania

Wote waligomea mpango huo kwa kile walichoeleza kuwa uongozi haukuwashirikisha
Hata hivyo ni kama uongozi wa Yanga umeridhia kuwarejesha kikosini kumaliza msimu licha ya kukosa mazoezi tangu dirisha la usajili lilipofungwa mwezi Januari
Akizungumzia kurejea kwa wachezaji hao, kocha msaidizi wa Yanga Charles Mkwasa amesema haoni tatizo kwa wao kushiriki mazoezi kwani ni wachezaji halali wa Yanga
"Sioni tatizo, hawa ni wachezaji wa Yanga. Mazoezi haya yatawasaidia kulinda viwango vyao ingawa sina uhakika kama wataruhusiwa kucheza mechi zilizobaki," alisema Mkwasa
Beki Mzanzibar Ali Ali amesema atahakikisha anatumia nafasi aliyopewa kulishawishi benchi la ufundi kuweza kumpa nafasi katika michezo iliyobaki
Amesema anajiamini, anao uwezo na yukjo tayari kuwania nafasi kwenye kikosi cha kwanza na wachezaji wengine
Kwa upande wa Lothi amesema yeye bado ni mchezaji halali wa Yanga hivyo kufanya mazoezi na timu ni wajibu wake