Pamoja na kukosekana uwanjani kwa zaidi ya miezi 18 kutokana na majeraha ya goti, winga wa Yanga Juma Mahadhi amerejea kikamilifu kwenye kikosi cha timu hiyo
Mahadhi ameshiriki mazoezi yote ya Yanga yanayosimamiwa na kocha msaidizi Charles Mkwasa tangu wiki iliyopita
Akizungumzia mwenendo wa nyota huyo, Mkwasa amesema Mahadhi ameonyesha uwezo mzuri licha ya kuwa alikaa nje kwa muda mrefu
Amesema mchezaji huyo yuko tayari kutumika na ameongeza ushindani katika nafasi anayocheza
"Taarifa ya madaktari imeonyesha yuko vizuri, nami kama kocha nimemruhusu kurudi kikosini na nampangia majukumu. Hadi sasa ameonesha uwezo mzuri hivyo yuko tayari kutumika," Mkwasa alinukuliwa na tovuti ya Yanga
Kwa mara ya mwisho Mahadhi kuonekana uwanjani ilikuwa August 19 2018 kwenye mchezo wa kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya USM Alger
Katika mchezo huo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, Mahadhi alipata majeraha hayo yaliyomuweka nje kwa karibu miaka miwili
Nyota huyo mwenye kasi ya 'kimbunga', ana kazi ya kurejesha 'fitness' yake baada ya kukaa nje kwa muda