Tambo baina ya watani wa jadi Yanga na Simba ndizo zinazonogesha upinzani wa kihistoria uliopo baina ya timu hizo kongwe zaidi nchini
Pamoja na kuwa katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita Simba imekuwa na mafanikio zaidi, lakini msimu huu hata kama Yanga itakosa ubingwa, ina jambo kubwa la kujivunia dhidi ya watani zao Simba
Ndio! Msimu huu Simba haiwezi kuwa na jeuri mbele ya Yanga kwani timu hiyo haikuweza kufua dafu katika mechi zote mbili walizokutana
Ushindi waliopata Yanga March 08 kwa bao Bernard Morrison, umeendeleza historia za kipekee kwenye mipambano baina ya timu hizo
Antonio Nugaz, Msemaji na Mhamasishaji wa Yanga ametamba kuwa tukio la March 08 limeingia katika historia ambayo kamwe haitafutika
"Kumbukumbu sahihi ambayo imeingia kwenye historia ambayo haitofutika. Sio tu kwamba tarehe 08/03/2020 tuliwafunga mbele ya marais watatu, lakini pia tuliweka historia ya mchezo wa nyumbani (Yanga Vs Wao) na kufanikiwa kuujaza Uwanja na Kuwa timu ya kwanza kuingiza mapato makubwa kwa serekali yetu pendwa ya Shilingi milioni 153.2 ambayo hayajawahi kupatikana Katika Mchezo ya Watani yote iliyopita"
"Hii ndio maana halisi ya Timu (Brand) inayopendwa na yenye mvuto kuliko timu yeyote Tanzania na Afrika Mashariki"
Lakini pia ushindi huo uliwaongezea kujiamini wachezaji ambapo wametamba kuwa katika mechi ambazo hazitawaumiza kichwa ni kukutana na Simba
Upo uwezekano timu hizo zikakutana kwenye nusu fainali ya kombe la FA kama Yanga itashinda mchezo wa robo fainali dhidi ya Kagera Sugar na Simba ikishinda mchezo wake dhidi ya Azam Fc
Habari njema ni kuwa tayari kocha wa Yanga Mbelgiji Luc Eymael amewasili kukiandaa kikosi chake akiwa na hesabu za kushinda taji la FA ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya CAF msimu ujao