Kwa sasa kwenye kikosi cha Yanga kuna mchezaji mmoja tu ambaye yuko na mabingwa hao wa kihistoria kwa muda mrefu
Sio mwingine ni mkongwe, Kelvin Yondani ambaye amedumu Yanga kwa zaidi ya misimu nane
Amedumu kwenye mikiki mikiki ya ligi kuu ya Tanzania Bara tangu mwaka 2006 huku akilinda kiwango chake kuwa katika ubora uleule
Nyota wanaocheza nae Yanga wamemzungumzia Yondani kama mchezaji wa kipekee ambaye anastahili kuheshimiwa. Lakini pia bado mchango wake unahitajika kwenye kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria
Kiungo Patrick Sibomana amesema ni heshima kubwa kwake kucheza na Yondani kwani alianza kumsikia tangu wakati yuko Rwanda
"Unajua Kelvin Yondani ni kama lejendi, nakumbuka wakati nipo Rwanda nilikuwa nasikia tu majina mawili kutoka Tanzania, yeye na Nadir Haroub 'Cannavaro'
"Kwa kipindi hicho nilikuwa siwafahamu, lakini sasa hivi nafurahi sana kucheza nae, anatufundisha mambo mengi sana kwa kuwa ana uzoefu mkubwa"
"Wakati mwingine tukiwa kwenye mechi huwa anatuambia kabisa kwamba, tunapaswa kupambana sana tunapokuwa ugenini kwa sababu ni mechi ambazo mara nyingi zinakuwa ngumu"
Naye mshambuliaji Yikpe Gnamien alimtaja Yondani kama mchezaji anayefahamu vyema majukumu yake anapokuwa uwanjani
"Asikwambie mtu, Yondani ni mchezaji mzuri sana, anajua nini cha kufanya na ni wakati gani wa kufanya jambo husika, lakini yule ni mzoefu kwa sababu amecheza hapa kwa muda mrefu, lakini kubwa zaidi ni kwamba, akiwa kazini anakuwa siriazi sana na huwa hataki masihara kabisa"
Maoni mengine yalitolewa na David Molinga ambaye amesema Yondani ni mchezaji anayepaswa kuheshimiwa katika kikosi cha Yanga
"Kwa upande wangu naweza kusema kuwa, Yondani ni mchezaji ambaye anahitaji kuheshimiwa kwa kiasi kikubwa, amecheza hapa kwa zaidi ya miaka kumi, sio mtu anaepaswa kulinganishwa na wachezaji wa kawaida, lakini tatizo waafrika wengi huwa hawatoi heshima kwa wachezaji wazuri kama alivyo Yondani"
"Yule ni mchezaji mzuri, mimi binafsi nafurahia kucheza nae, ana vitu vingi ambavyo mabeki wengine hawana, hilo nakuhakikishia kwa kuwa nimecheza sehemu mbalimbali Afrika"
Moro akamtaja Yondani kama mmoja wa mabeki bora ambao amewahi kucheza nao timu moja katika maisha yake ya kusakata kabumbu
"Ni kweli nimecheza na walinzi wengi katika timu nyingine kabla sijaja Yanga, lakini kucheza na Yondani ni maajabu kwa kuwa yule ni mtu mzuri, yupo makini sana anapokuwa kazini na hapendi mzaha.
"Mimi naona Yondani ni mchezaji anaepaswa kuigwa na wachezaji wengi vijana ambao ndio wanaanza kujikita kwenye Soka hususani kwa wachezaji vijana wanaochipukia" .
Kwa upande wa Tshishimbi yeye alieleza kushangazwa na maisha anayoishi mchezaji huyo ambayo yanamfanya kuwa huru kukaa mahali popote
"Unajua kuna vitu vinanichekesha, nikimtazama Yondani huwa sipati jibu sahihi. Yani yule jamaa anaweza kuishi mahali popote, kwenye kundi la wahuni ukimuweka anakaa, kundi la watu wapole anaweza kukaa na hata kwenye kundi la watu wabishi unaweza kumuweka"