Baada ya mchezo dhidi ya Azam Fc ambao ulimalizika kwa suluhu ya bila kufungana, ni dhahiri mabingwa wa kihistoria Yanga watahitaji mabadiliko makubwa kama wanataka kurejea wakiwa imara msimu ujao
Pamoja na kumiliki mchezo wa nyakati tofauti, timu ilikosa mbinu za kuipenya safu ya ulinzi ya Azam, lawama zikitupiwa washambuliaji Patrick Sibomana, Ditram Nchimbi na David Molinga ambao hata nafasi chache walizopata hawakuzitumia
Eneo la ushambuliaji linaweza kuwa la kwanza katika maboresho ambao yanapaswa kufanyika. Ni vizuri hata viongozi wa Yanga wametambua changamoto hiyo na kutoa kipaumbele kwa usajili wa washambuliaji
Eneo la kiungo mkabaji pia linaonekana kuwa changamoto hasa pale anapokosekana Mcongmani Papy Tshishimbi ambaye ni nahodha wa timu hiyo
Jana Azam Fc walitumia madhaifu ya Yanga katika eneo hilo ambalo lilikuwa chini ya Feisal kuifikia kwa urahisi ngome ya Yanga na kama washambuliaji wake wangekuwa makini, wangepachika mabao zaidi ya mawili
Usajili wa washambuliaji wa pembeni nao unapaswa kuwa kipaumbele. Ni vizuri kusikia tayari Yanga imemnasa Tuisila Kisinda kutoka AS Vita lakini bila shaka watahitaji kusajili angalau washambuliaji wawili wa pembeni ambao uwezo wao uko katika kiwango cha Bernard Morrison
Wakati mwingine safu ya ushambuliaji inaweza kuonekana haifanyi vizuri lakini pengine ni kutokana hakuna watu wa kuwatengeneza nafasi za kufunga mabao
Timu inapokuwa na mawinga wazuri pamoja na viungo, kunakuwa na uhakika wa kutengeneza nafasi nyingi
Enzi za kina Saimon Msuva, kina Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Obrey Chirwa walifunga mabao vile walivyotaka kwani timu ilikuwa ikitengeneza nafasi nyingi kupitia pembeni
Yanga haionekani kuwa na changamoto sana katika eneo lake la ulinzi, Said Juma Makapu kwa sasa anaonekana kuiva na anaweza kuwa mbadala wa Yondani pale atakapotangaza kustaafu
Aidha, ujio wa Erick Rutanga nao unakwenda kuimarisha eneo la ulinzi upande wa kushoto ambalo kwa sasa liko chini ya Jaffar Mohammed ambaye kwa kiasi kikubwa amekuwa akifanya vizuri ingawa wakati mwingine amekuwa akijisahau kwa kuwa namba tatu sio asili yake
Viongozi wa Yanga pamoja na wadhamini GSM wanapaswa kufanya usajili ambao utazingatia mapendekezo ya Mwalimu na wenye lengo la kumaliza changamoto zinazoonekana kwenye kikosi cha Yanga